2014-06-21 08:40:34

Onja siri ya mafanikio!


Mkataba ni “makubaliano yanayofikiwa kwa kuandikiana baina ya watu au vikundi viwili au zaidi ili kufanya jambo au kazi fulani.” Kitega uchumi (investment) ni “raslimali kama vile duka, kiwanda inayotumika kuzalisha mali” na Mwekezaji ni “mtu anayewekeza fedha au mali katika biashara au mradi fulani.”


Maneno haya matatu Mkataba, Kitegauchumi na Mwekezaji yanatumika sana katika ulimwengu wa leo wa uchumi. Jambo muhimu kabla ya kutiliana sahini na mwekezaji, ni budi kutathmini kwa kina vikwazo vyote vinavyoweza kuyumkinika. Leo tutapata ushauri nasaa wa kutusaidia kusahini mikataba nyeti ya uwekezaji. Ukifuatilia kwa dhati masherti ya mkataba wa Mwekezaji mkuu wa leo, ninakuhakikishia utafaulu tu katika maisha yako.


Injili ya leo ya Yohane ni mafundisho ya Yesu akiwa ndani ya Sinagogi ya Kafarnaum. Kabla yake, Yesu aliwalisha chakula halaiki ya watu kwa muujiza wa kuongeza mikate na samaki. Matokeo ya awali ya muujiza huo yaliwaachamisha watu midomo wakimtaka awe kiongozi wao: “Watu walipoona ishara ile, wakaamua kumteka kuwa mfalme wao” (Yoh 6:14-15). Tunajiuliza, kulikoni, halaiki hii ya watu kushikwa butwaa na kutaka kumpa Yesu uongozi kwa harakaharaka hivyo? Jibu linaweza kuwa labda kwa sababu wamemwona anayo nguvu ya Kimungu, au labda alitaka kuandaa mazingira ya kuwekeza katika chakula. Kama ndivyo, basi halaiki hii ilikuwa katika hatari ya kunaswa katika mtego unaowanasa wengi.


Mosi, kama sasa Yesu angetaka watiliane mkataba juu ya uwekezaji katika chakula (mikate na samaki), hapo sahini zingepigwa kwa ulaini. Kadhalika angetaka kuomba kura ya imani juu yake kama mwekezaji, mkataba huo nao ungepita kirahisi lakini bila kuujua sawasawa, kwa sababu watu hawa walishahamasika katika imani isiyokomaa. Walimshabikia Yesu kwa sababu ya samaki na mikate.


Pili, yaoneka hawakutafakari kwa kina na kujua malengo ya Yesu ya kuwalisha chakula hicho. Kumbe imani komavu ni ile inayomwelewa Yesu kuwa hafanyi miujiza ili kushangaza na kuvuta mashabiki, bali ina lengo la kuonesha umaana na uhalisia wa ndani wa maisha. Kwa mfano, kwa uponyi wa kipofu kutoka kuzaliwa kwake, mwamini wa kweli anamwona Yesu anayejidhihirisha kuwa mwanga au nuru ya dunia.


Katika muujiza wa kugeuza maji kuwa divai unamgundua Yesu kuwa ni chemchemu ya furaha ya kweli; katika kumhuisha Lazaro unamwelewa Yesu kuwa ni Bwana wa maisha; na katika kuwalisha mikate wenye njaa unamwona Yesu kuwa chakula kisichoisha. Namna hiyo ndiyo anayotaka Yesu ya kuelewa kwa kina miujiza na mikataba yake. Kumbe Kafarnaumu watu wameangalia matukio kwa nje tu. Halaiki hii inahitaji kusaidiwa kufanya utafiti na kupambanua kati ya “chakula kinachoangamiza” na “chakula kinachodumu daima” (Yoh. 6:27).


Kwa hiyo baada ya kuwateka watu kwa chakula, Yesu anatoa maelezo ya kina juu ya mswada wa makubaliano akijipendekeza yeye kuwa ndiyo mwekezaji mkuu na anajiwekeza mwenyewe, yaani Yeye mwenyewe ni kitegauchumi na ni mwekezaji. Anasema waziwazi: “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni” (Yoh. 6: 33-35). Kwa wayahudi chakula kilichoshuka kutoka mbinguni kilikuwa ni manhu au mana (Zab. 78:24), na chakula kinacholisha walielewa kuwa ni Neno la Mungu au Maandiko Matakatifu (Isaya 55:1-3).


Yesu anapojitangazia kuwa yeye ni chakula kutoka mbinguni yamaanisha yeye ni Neno la uhai, na anayemsikiliza anajilisha Neno la uzima. Kwa tamko hilo wayahudi wakaanza kuuhoji na kuukosoa mswada huo: Anawezaje huyo, “mtoto wa Yosefu” kuzungumza lugha kama hii – Anajidai kuwa nani? (Yoh 6:42). Angalia pia kashfa za Mama msamaria: “Wewe unajidai labda kuwa mkubwa zaidi ya Baba yetu Yakobo?” (Yoh 4:12).


Baada ya kashfa hizi zote, tungetegemea Yesu labda angerekebisha baadhi ya vipengele vya mswada, kumbe kinyume chake anaendelea kutoa masherti mazito zaidi, yaani sasa chakula hicho siyo mafundisho yake tu, bali ni nyama yake hasa. Anasema: “Na chakula nitakachotoa mimi ni nyama yangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” (Yoh 6:51). Hayo ndiyo maneno ya mwanzo wa Injili ya leo.


Kusudi tusigongane lugha na kuanza kuzingiziana uchawi kuhusu kula nyama ya Yesu, ni budi ieleweke kwamba Biblia inapozungumzia juu ya nyama haimaanishi kula misuli na steki, la hasha, bali humaanisha udhaifu, unyonge, udogo, hali ya kufa na kuoza ya binadamu. “Bwana akasema, ‘Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.’” (Mwa 6:3).


Aidha mbele ya matatizo ya maadili ya wayahudi, mzaburi anamkumbuka Mungu anayejizuia asiwawakie hasira wayahudi kwa vile “Akakumbuka kuwa wao ni kiwiliwili (nyama), upepo upitao wala haurudi.” (Zab 78:39). Nyama ina maana ya kujishusha, kujinyenyekea kwa Mwana wa Mungu hadi kufikia kiwango cha chini kabisa cha udhaifu wa binadamu kwa umwilisho wake. “Naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu.” (Yoh 1:14). Kwa hiyo kumla Mungu aliyekuwa mwili, maana yake kutambua ufunuo wa Mungu aliyefikia ulimwenguni kwa njia ya “Mwana huyu wa mseremala” na kuipokea hekima hii iliyoshuka kutoka mbinguni.


Wayahudi walitambua kwamba Yesu hakusemea tu kule kupokea mawazo au mafundisho ya kiroho ambayo ni ufunulio wa Mungu, bali pia “kula nyama hasa,” ndiyo maana wanahoji: “Awezaje mtu huyu kutupa sisi mwili wake ili tuule?” (Yoh 6:52). Yesu hajali mshangao wao, sasa anaendelea kusisitiza zaidi umuhimu siyo tu wa kula nyama yake, bali hata wa kuinywa damu yake kabisa (Yoh 6:52-56).


Biblia inakataza kunywa damu “Kila mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, atakayekula damu ya aina yoyote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.” (Mambo ya Walawi 17:10-11). Damu ni alama ya uhai, uzima, maisha. Maisha na uzima wote ni wa Mungu. Kunywa damu maana yake ni kuyapokea kabisa maisha ya Yesu.


Kutoka katika kipengee hiki sasa tunaingizwa kwenye Mkataba unaohusu mradi mkuu wa Yesu wa kujiwekeza mwenyewe katika Mkate na Divai, yaani Ekaristi Takatifu. Kabla ya kueleza maana ambayo katika fikra za Yesu alitaka kuizungumzia Sakramenti hiyo ambayo ni “msingi na kilele cha maisha yote ya mkristu”, ingefaa tukiweze wazi kipengee kimoja cha kiibada juu ya Ekaristi jinsi kisivyo na uhusiano wowote na maana ya kibiblia.


Lengo kuu la Yesu la kuweka Ekaristi Takatifu ni kwa ajili ya kuliwa: “Twaeni mle wote, huu ndiyo mwili wangu. Twaeni mnywe wote, hii ndiyo damu yangu”. Kwa hiyo hata kama Ekaristi inawekwa altareni kwa ajili ya kuabudiwa yatakiwa chombo kilimowekewa Ekaristi kioneshe waziwazi kwa nje kuwa ndani mwake kuna chakula cha kuliwa nacho ni Yesu Kristu mwenyewe, mwili na damu yake katika umbo la mkate na divai.


Aidha ni budi ieleweke kuwa tunapozungumzia juu ya uhakika wa kufikia umoja wa maisha na Kristu, inatosha kuwa na imani juu ya Neno lake, yaani kuisoma na kuishika Biblia, zoezi linalofanyika na watu wengi sana. Kutokana na kujilisha Neno la Mungu, tunapata uzima wa Mungu. Kama tunavyosoma: “Yeye aaminiye yuna uzima wa milele.” Yoh 6: 47). Kadhalika Yesu alisema “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele” (6:54). Hapa unaona wazi kwamba matokeo ya kusikiliza Neno na yale ya kula mwili ni yaleyale. Kwa hiyo ingetosha tu kulisikiliza Neno lake.


Kwa maana hiyo inafaa hata sisi leo kujihoji: Kuna umuhimu gani wa kutilia sahihi kupokea komunio takatifu? Kwa sababu gani Yesu ametupatia mradi mgumu wa kula nyama yake na kunywa damu yake katika umbo la mkate na divai? “Kula mwili wake na kuinywa damu yake”. Ndilo wazo muhimu sana tunalotakiwa kulifanyia tafakuri.


Ndugu zangu, tumeona kuwa mapato ya kusikiliza Neno ni sambamba na yale ya kupokea Komunio takatifu. Kifanyikacho mara zote katika Misa takatifu ni kwanza kusikiliza masomo ya Biblia. Neno la Mungu ni kipengee muhimu sana cha kutuelimisha kabla ya kupokea Ekaristi Takatifu.


Yaani, kuelewa kwanza kuwa anayekubali kuwa nafsi moja na Kristo katika sakramenti, huyo hana budi atambue waziwazi mapendekezo anayotoa Kristu na budi achukue maamuzi ya dhati ya kuyapokea na kuyaishi. Kama anavyoonya vikali sana mtume Paulo: “Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili.” (I Kor. 11:28-29). Tendo la kupokea mwili na damu ni la maamuzi ya dhati ya mtu binafsi. Mathalani tendo la kunyosha mkono au kufungua mdomo na kutoa ulimi kupokea mkate uliowakfiwa, ni tendo binafsi la ndani kabisa ya mtu ya kumpokea Kristu na ya kuitikia kwamba mawazo yake yawe mawazo yetu, maneno yake yawe maneno yetu, uchaguzi wake uwe ndiyo uchaguzi wetu. Katika Ekaristi, nafsi ya Yesu inakubalika kama inavyoonekana katika mkate na divai.


Mabadiliko yatokanayo na kuamini hivyo hufika polepole, nayo yataonekana katika kufaulu au kushindwa, lakini kusikiliza kwa unyenyekevu Neno na tendo la kupokea komunio ndilo linalofanya muujiza. Huo muujiza utatokea tu siku moja kwa wafuasi wake wanaompokea katika komunio. Watayafurahia mabadiliko hayo yatakayopatikana kutoka Roho anayefanya kazi na hatimaye watasema kama Paulo: “Sasa lakini wala si mimi tena, bali Kristu yu hai ndani yangu” (Gal 2:20).


Aidha, kwa vile chakula anachotupatia Yesu ni nafsi yake mwenyewe, tunapokula chakula hicho kinatufanya tukutane, tufurahi, tuwe na nguvu, tuwe na mang’amuzi mapya ya maisha. Kumla Yesu maana yake kufungua mlango wa uwepo halisi katika mwili na damu ya Neno la milele la Mungu, kulifanya liingie na kuzama ndani ya akili na fikra zako ili ziweze kuangazwa na fikra zake. Nyama na damu yake ifanye makao yake na iwe kitivo chetu.


“Anayemla Yesu anayo maisha ya milele.” Unaweza kujadili unavyotaka wewe ukweli wa maneno hayo, lakini kama hujilishi na Kristu, basi maisha yamekushinda, unakufa polepole kwa sababu upo kwenye mteremko mkali wa mitego mingi ya kifo. Jaribu kupata picha rahisi tu ya muujiza huu, kwamba kwa kupokea kakipande kadogo kabisa ka mkate, yaani hostia ile iliyobarikiwa: Mbingu yote ikiwa pamoja na Yesu inaingia ndani ya moyo wako na hivi mtima wako unakuwa mbingu. Wanakuja na kukaa ndani yako wapendwa wote ambao hawapo tena katika dunia hii ambao wapo pamoja na Yesu.


Kwa Komunio unayopokea unapata fursa ya kujisikia kuunganisha dunia na mbingu, unajizamisha katika Upendo wa milele na kuukumbatia na unakumbatiwa na yule anayefurahia maisha ya heri. Tungetambua kwa undani wake neema iliyojificha ndani ya vipande vile vitakatifu vya komunio takatifu, tungewania kila siku kujongea altareni na kupokea komunio. Neno linakufanya upya, Ekaristi inakuhuisha na kukufanya uishi.


Ukijaribu utaamini. Akili yako inapanuka, mawazo yanaangazika, kila kitu kinakuwa na mtazamo linganifu wa mambo na kuweza kukabili maisha ipasavyo. “Ukitaka kujua utamu wa ngoma ingia kucheza”. Ndiyo, kwa vile utaishi katika maisha ya Mungu utapunguza matatizo na utapata matumaini. Anayemla Yesu anaishi kwa ajili yake hawezi kufanya kinyume cha anavyofanya Yeye. Mwekezaji huyu hadanganyi wala hadanganyiki. Tunahimizwa kutilia sahihi mkataba wa Yesu aliyejiwekeza mwenyewe katika Ekaristi Takatifu. Tumpokee kwa moyo safi. Heri sana kwa sikukuu ya Ekaristi Takatifu.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.