2014-06-21 10:24:45

Jubilee ya miaka 50 ya Kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Moyo Mtakatifu wa Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kitivo cha Tiba na Upasuaji cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kilichoko mjini Roma, sanjari na Siku kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, siku ambayo imetengwa maalum kwa ajili ya kuombea Utakatifu wa Mapadre, atatembelea na kusali pamoja na Majaalimu, wafanyakazi, wanafunzi na wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Gemelli.

Kitivo cha Tiba na Upasuaji, kiko chini ya maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku kuu ambayo itaadhimishwa Ijumaa, tarehe 27 Juni 2014. Baba Mtakatifu Francisko alionesha nia hii na kuitangaza hadhari tarehe 4 Mei 2014 wakati wa maadhimisho ya Siku ya 90 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Ratiba elekezi kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko inaonesha kwamba, atawasili Hospitalini hapo majira ya Saa 9:30 Alasiri na kupokelewa na viongozi wakuu wa Hospitali. Atasalimiana na wagonjwa watakaokuwepo kwenye Uwanja wa Hospitali na wale watakaokuwa wanaangalia kupitia kwenye madirisha ya Wodi zao. Lakini atapata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wagonjwa kwenye chumba maalum Hospitalini hapo.

Baba Mtakatifu baadaye, atakwenda moja kwa moja kwenye Kikanisa cha Moyo Mtakatifu wa Yesu kutoa heshima zake za dhati kwa Masalia ya Watakatifu Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II. Hapa Baba Mtakatifu anatarajiwa kutoa hotuba kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Majira ya saa 11: 30 Jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Baada ya Misa Takatifu, Kardinali Angelo Scola, Rais wa Taasisi ya Toniolo pamoja na Professa Franco Anelli mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu watatoa neno la shukrani. Baba Mtakatifu atatembelea taasisi ya bayolojia na kuzungumza na wahusika na baadaye, atahitimisha hija yake Chuoni hapo.







All the contents on this site are copyrighted ©.