2014-06-21 18:01:04

Furaha ya Upadre inafumbatwa katika umoja na udugu!


Baba Mtakatifu Francisko majira ya mchana, Jumamosi tarehe 221Juni 2014, akiwa Jimboni Cassano Allo Jonio, Calabria, Kusini mwa Italia, amekutana na kuzungumza na Mapadre wanaotekeleza utume wao Jimboni humo, ili kuwashirikisha na kuwamegea ile furaha ya kuitwa na Yesu ili kuwa Padre, furasa ya kuweza kuitafakari kwa kina ile sura ya Yesu mbele ya Tabernakulo katika hali ya ukimya, ili kutambua kwamba, Yesu anawapenda, anawapyaisha na kuwapatia moyo mkuu wa kuweza kusonga mbele katika maisha na utume wao!

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, si rahisi kuketi daima mbele ya Yesu kutokana na shughuli mbali mbali zinazowakabili katika maisha na utume wao kama Mapadre. Lakini wakati mwingine sura ya Yesu inawasuta na katika ukimya wa sala Yesu anawasaidia kutambua ikiwa kama kweli wanatenda kama wafanyakazi bora, mikono ya watu ambao Mwenyezi Mungu anaitumia ili kuwapatia watu wake neema na baraka, au Mapadre hawa wamebadilika na kuwa ni watu wa mshahara, watu ambao wanaojitafuta wenyewe na kwa ajili ya mafao yao binafsi. Ni watu ambao wamekuwa ni ukuta unaowazuia wengine kukutana na Yesu, kiasi kwamba, wanashindwa kuuona mwanga na nguvu ya Injili!

Baba Mtakatifu Francisko amewashirikisha Mapadre uzuri wa mshikamano wa udugu katika maisha na utume wa Kipadre, kwa kumfuasa Kristo, kila Padre akijitahidi kushirikisha karama na pamaji yake, kielelezo kikubwa cha maisha ya Kipadre yanayojionesha hata katika utofauti wa umri na karama, lakini yote ni kwa ajili ya kujenga umoja na mshikamano wa kidugu katika maisha na utume wa Kipadre.

Baba Mtakatifu anasema, hata hapa mambo si rahisi kama wanavyodhani baadhi ya watu, kwani kila mtu ana mwelekeo na mitazamo yake kiasi kwamba, utamaduni mamboleo unataka watu wajikuze, hali inayopelekea ubinafsi kutawala zaidi, kumbe kuna haja ya kujikita katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kidugu. Maamuzi mbali mbali hayana budi kupokelewa na kukuzwa, ili kujenga umoja na Kristo kwa kushikamana na Askofu mahalia.

Baba Mtakatifu anasema dhana hii inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa Jimbo husika mintarafu shughuli za kichungaji, mwelekeo wa kimissionari na upendo kati yao na hatimaye, kuhakikisha kwamba, upendo huu unasambazwa kwa Familia ya Mungu wanayoihudumia.

Furaha ya kuwa Padre inakamilishwa na umoja na udugu unaojionesha katika maisha na utume wa Kipadre; mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu amependa kuwashirikisha Mapadre kutoka Jimbo Katoliki la Cassano allo Jonio, lililoko Kusini mwa Italia. Anawahimiza kuendelea kutekeleza utume wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia na kwa ajili ya familia, kwani hii ndiyo changamoto kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwawajibisha kutokana na ukweli kwamba, Familia katika ulimwengu mamboleo zinakabiliana na changamoto nyingi.

Baba Mtakatifu anasema, pale ambapo mambo yanayoonekana kuwa magumu zaidi, hapo ndipo Mwenyezi Mungu anapoonesha uwepo wake wa karibu, neema na nguvu za kinabii kwa ajili ya familia. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru Mapadre kwa makaribisho, wema na upendo waliomwonjesha wakati wa hija yake ya kichungaji Jimboni humo!







All the contents on this site are copyrighted ©.