2014-06-21 17:59:32

Ekaristi Takatifu ni Sherehe ya Kuabudu na Kushukuru!


Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanapania kumshangilia Yesu Kristo Mkate ulioshuka kutoka mbinguni. Kanisa linamshukuru Yesu kwa zawadi kubwa ya Fumbo la Ekaristi Takatifu lililoanzishwa na Yesu mwenyewe Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake.

Hii ni Sherehe inayoonesha moyo wa shukrani na ibada kuabudu Ekaristi Takatifu inayotembezwa mitaani, kuonesha imani ya Wakristo wanaotembea na kumwabudu Yesu; mambo msingi katika Sherehe ya Ekaristi Taktifu. Wakristo watambue kwamba, wao ni watu wanaojipambanua kwa kumwabudu Mwenyezi Mungu, chemchemi ya upendo iliyofunuliwa kwao kwa njia ya Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Upendo wa Yesu unaendelea kujionesha ndani ya Kanisa.

Waamini wanaonesha imani yao kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa kumkataa Shetani na mambo yake yote, kwa kuyatakaa malimwengu na fahari zake zinazojionesha katika uchu wa mali na madaraka; mambo yanayomjengea mwanadamu kiburi! Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kumwabudu Yesu peke yake, anayeonesha uwamo wake endelevu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, mwaliko kwa waamini kutambua imani wanayoiungama katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wamwombe Kristo ili awapatie mwanga na neema ya toba na wongofu wa ndani, ili kweli waamini waweze kumwabudu Yesu Peke yake na wala si vinginevyo!

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu, Sherehe ya Ekaristi Takatifu kwenye Jimbo Katoliki la Cassano allo Jonio, Calabria, Kusini mwa Italia, Jumamosi jioni, tarehe 21 Juni 2014. Kanisa linaungama imani kwa Yesu Kristo: Mungu kweli na Mtu kweli; ambaye yumo katika maumbo ya mkate na divai, anayewachangamotisha waamini kujibidisha kufanya hija pamoja naye, huku wakitekeleza ile amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Watambue kwamba, wao ni watu wanaomwambudu Mungu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, watu wanaofanya hija katika upendo.

Baba Mtakatifu anasema, yuko kati yao ili kuwaimarisha katika msingi wa imani na mapendo pamoja na kuendelea kuwatia shime katika hija wanayoifanya pamoja na Yesu chemchemi ya upendo. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Makleri wanaotekeleza utume wao Jimboni Cassano na Calabria katika ujumla wake. Makleri hawa wanaendelea kujisadaka kwa ujasiri katika utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa njia ya mtindo wa maisha unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu anawashukuru viongozi wa Kisiasa na Serikali wanaotekeleza wajibu wao kwa kuzingatia kwanza kabisa mafao ya wengi, kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma. Anawataka waamini na wananchi wote wenye mapenzi mema, kutolea ushuhuda unaojikita katika maisha ya watu, kwa kukazia haki, matumaini na huruma. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na familia zao kwa kuonesha alama za matumaini zinazobubujika kutoka ndani ya familia zao, parokia na vyama vya kitume. Yesu katika hija na wafuasi wake ataendelea kuamsha ndani mwao alama za matumaini kwa vijana ili wawese kujisadaka kwa ajili yao na jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena anawataka vijana kutokubali kupokonywa matumaini waliyo nayo! Waendelee kumwabudu na kuungana na Yesu Kristo na kwa njia hii, wataweza kupingana na dhambi, ukosefu wa haki, matumizi ya nguvu, kwa kujikita katika kutafuta kilicho chema, kizuri na kweli.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kifungo cha umoja na upendo, kinachowaunganisha waamini kuwa kweli ni Familia moja; Watu wa Mungu wanaoungana kumzunguka Yesu, Mkate wa uzima wa milele. Kwa kufanya hija na Yesu, Kanisa la Kijimbo na Parokia zitaweza kukua na kushamiri katika imani, upendo na furaha katika mchakato wa Uinjilishaji. Hili litakuwa ni Kanisa linalojengeka katika mshikamano wa upendo miongoni mwa watu wake, kwa kusaidiana na kupendana kama ndugu, hasa nyakati za magumu na mahangaiko ya ndani.

wakati huo huo, Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kutekeleza ahadi ya kuwatembelea, ili kukutana na Kanisa ambalo linajipambanua kwa utume na ukarimu; watu wanaotaka kufanya mabadiliko katika maisha yao, ili kujijengea uwezo wa kiuchumi pamoja na kupambana na vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu kama vile "Ndragheta". Majiundo makini yanayotolewa kwa waamini yanapania kuamsha tena dhamiri nyofu, ili kutangaza na kuishuhudia Injili ya Furaha.

Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuomba msamaha, lakini Askofu Galantino kwa upande wake anaomba pia msamaha kwa kutowaonjesha watu wake huruma na msamaha. Anawakumbatia Makleri, Watawa na wagonjwa wote wa Jimbo lake.All the contents on this site are copyrighted ©.