Andaeni sera na mikakati ya maendeleo inayotekelezeka!
Askofu mkuu Seraphin Rouamba, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso na
Niger anaitaka familia ya Mungu katika nchi hizi mbili kujikita katika mikakati ya
shughuli za kichungaji itakayojenga na kuimarisha utamaduni wa maendeleo endelevu
ya binadamu, kwa kuzingatia mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.
Askofu
mkuu Rouamba ameyasema hayo wakati alipokuwa anafungua mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu
katoliki Burkina Faso na Niger, hivi karibuni, katika Kituo cha Kimataifa cha Kardinali
Paul Zoungrana, kilichoko mjini Ouagadougou. Maaskofu wamepata fursa ya kusikiliza
taarifa za shughuli mbali mbali zinazofanywa na Tume za Mabaraza ya Maaskofu huko
Burkina Faso na Niger.
Askofu mkuu Rouamba anasema kuwa, huduma kwa Familia
ya Mungu ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki, kwani linatumwa na Kristo kumhudumia
mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa Kanisa kwa kushirikiana
na wadau mbali mbali kupembuana kubainisha miradi ya maendeleo endelevu inayotekelezeka
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Barani Afrika.
Mwishoni,
Maaskofu wamewaomba waamini na wananchi katika ujumla wao kuendelea kuombea amani
na upatanisho wa kitaifa huko Burkina Faso na Niger.