2014-06-20 12:09:58

Utajiri wa kweli unajionesha kwa mapendo kwa Mungu na jirani!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Siku ya Ijumaa tarehe 20 Juni 2014 anasema kwamba, Neno la Mungu linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujitafutia utajiri wa kweli unaogusa undani wa mtu kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha pamoja na kuwasaidia jirani. Lakini kwa bahati mbaya, watu wa dunia hii wanapenda kujilimbikizia fedha na mali, mambo ambayo yanaweza kuibiwa au kuliwa na mchwa!

Baba Mtakatifu anasema watu waliojishikamanisha mno na fedha kiasi cha kujiwekea kiasi kikubwa cha fedha Benki na katika vitega uchumi, lakini wamejikuta hawana tena furaha ya kweli baada ya fedha zao kuibwa na vitega uchumi kuporomoka, kama inavyojionesha wakati huu kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Utajiri wa kweli uwasaidie waamini kutenda matendo mema, kwa kuzisaidia familia na jirani kuwa na maisha bora zaidi. Watu wasiweke matumaini yao yote katika mali na fedha anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Waamini wawe makini katika kujionesha mbele ya watu na kutafuta ufahari wa mpito, kwani mambo haya ni dalili za mtu kumezwa na malimwengu. Watu wanapenda madaraka kupita kiasi, lakini wanasahau kwamba, hata watu mashuhuri wamejikuta madaraka yao yakiingia "mchanga" na matokeo yake wakabaki watupu! Ufahari wa mambo ya dunia, madaraka na mali si msingi wa matumaini ya mwamini, watu wajitahidi kujiwekea hazina mbinguni kwa kuwa na mioyo huru.

Baba Mtakatifu anasema moyo wa mtu ambaye ni huru hakumezwa na malimwengu unajionesha kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu na mapendo kwa jirani. Hapa mwamini ataweza kuona ile njia inayokwenda mbinguni kwenye makao ya uzima wa milele. Ni mwamini ambaye ataweza kufurahia uzee wake na mwisho kuuona mwisho mkamilifu. Ni mtu anayechagua kwa kuzingatia vipaumbele vya maisha, busara na maongozi ya maisha ya kiroho, mfano bora wa kuigwa na Watoto wote wa Mungu!







All the contents on this site are copyrighted ©.