2014-06-20 08:59:46

Unataka kujishibisha kwa harufu ya masufuria ya nyama na vitunguu swaumu utumwani?


Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Mwili na Damu Azizi ya Kristo, iliyofanyika mjini Roma, siku ya Alhamisi, tarehe 19 Juni 2014 ameongoza Ibada ya Misa takatifu na baadaye maandamano ya Ekaristi Takatifu kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hadi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma. Waamini wamefanya maandamano haya kwa kusindikizwa kwa nyimbo, sala na tafakari ya Neno la Mungu na hatimaye, kuabudu Ekaristi Takatifu, tukio ambalo limewashirikisha maelfu ya waamini kutoka ndani na nje ya Roma.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu aliwaongoza Waisraeli Jangwani kwa kipindi cha miaka arobaini akawalisha kwa manna iliyoshuka kutoka mbinguni hadi siku ile walipoingia kwenye Nchi ya ahadi, wakaonja uhuru na kuanza kusahau shida na mahangaiko waliyokumbana nayo walipokuwa utumwani Misri. Waisraeli wanahimizwa kufanya kumbu kumbu ya safari yao ya miaka arobaini Jangwani, ili waweze kuzingatia mambo msingi kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, mtu hawezi kuishi kwa mkate tu, bali kwa kila jema linalotoka katika kichwa cha Bwana.

Baba Mtakatifu anasema mwanadamu ndani mwake ana njaa ambayo haiwezi kamwe kugangwa na chakula cha kawaida. Hii ni njaa ya uhai, upendo na maisha ya uzima wa milele, mambo msingi yaliyokuwa yamefumbatwa katika manna waliyokula Waisraeli Jangwani. Katika Agano Jipya, Yesu anajitoa mwenyewe kuwa Chakula hai kinachoupatia ulimwengu maisha mapya. Mwili wake ni chakula kweli na Damu yake ni kinywaji safi. Hiki ni chakula ambacho kinamkirimia mwanadamu: uhai, maisha ya uzima wa milele kwani ni chakula ambacho kinafumbata upendo.

Baba Mtakatifu ameuambia umati mkubwa wa waamini uliokuwa umefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwamba, Yesu anawashibisha waja wake kwa upendo wake mkamilifu, ili kupata nguvu mpya. Haya ni mang'amuzi ya imani yanayomtaka mwamini kujiachilia mikononi mwa Yesu ili aweze kumshibisha ili hatimaye aweze kujijenga kwa kutumainia karama za Mungu, Neno la Mungu pamoja na Mwili wa Kristo yaani Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wakichunguza kwa ukamilifu watangua kwamba, wamezungukwa na chakula ambacho hakishibishi kamwe, kwani baadhi ya watu wanapenda kujishibisha kwa kupenda mno fedha na mali, mafanikio ya haraka, madaraka na kiburi. Lakini waamini wakumbuke kwamba, chakula kinachowashibisha na kukata njaa na kiu ni kile kinachotolewa na Yesu.

Pale waamini wanaposhindwa kupata radha safi ya chakula hiki matokeo yake ni kuanza kutamani masuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu walipokuwa utumwani Misri, wakasahau kwamba, huko walikuwa ni watumwa. Hii ni kumbu kumbu potofu, kumbu kumbu inayochagua kwa kubanwa na kongwa la utumwa na kamwe haiwezi kumweka mwamini huru!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujiuliza ni wapi wanapotaka kushibishwa, mezani kwa Yesu au utumwani na kwamba, kila mwamini mmoja mmoja ana kumbukumbu gani katika maisha yake! Je, ni ile ambayo inamwonesha Yesu anayekomboa au bado anasikia harufu ya masuria ya nyama na vitunguu swaumu? Waisraeli walikumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu aliwalisha manna kutoka mbinguni, changamoto kwa waamini kuwa na kumbu kumbu hai na ya kweli, ili kutambua chakula kilichoharibika ambacho ni matunda ya ubinafsi, dhambi na kujiamini kupita kiasi.

Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, maandamano ya Ekaristi Takatifu yanaonesha uwamo wa Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, manna mpya inayomlinda mwamini dhidi ya dhambi na vishawishi vinavyomfanya kuwa mtumwa. Yesu anasafisha kumbu kumbu, ili kuondokana na ubinafsi pamoja na hali ya kumezwa na malimwengu. Yesu anataka kumbu kumbu hii iwe ni endelevu inayoonesha uwapo wake katika historia ya watu wake inayojikita katika upendo unaokoa!







All the contents on this site are copyrighted ©.