2014-06-20 08:15:28

Tunaomba msamaha!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji Jimboni Cassano all’Jonio liliko Kusini mwa Italia hapo tarehe 21 Juni 2014, wakati wa maandalizi ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu. RealAudioMP3

Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema kwamba, Baba Mtakatifu atapata fursa ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu majira ya jioni saa 11:00 kwa saa za Ulaya.

Waamini wanatambua zawadi kubwa ambayo Baba Mtakatifu anatarajia kuwapatia kwa kuwatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, ili wao pia waweze kuwa kweli ni Ekaristi kwa ajili ya jirani zao, hasa wakati huu Mama Kanisa anapojikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaodai ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Jimbo hili linaundwa na Jumuiya ndogo ya waamini, ni eneo ambalo linaweza kusahauliwa ki-urahisi, lakini imeonekana kuwa na thamani kubwa machoni pa Baba Mtakatifu Francisko, kiasi hata cha kumteuwa Askofu wake Nunzio Galantino kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Baba Mtakatifu alisema anapenda kuwatembelea ili kuwaomba waamini msamaha kwa kuwaondolea Askofu Nunzio Galantino, kipenzi chao kwa kumpatia utume mwingine! Kumbe, maandalizi ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Jimboni Cassano All’Jonio inaongozwa kwa kauli mbiu “Hata sisi tunaomba msamaha”.

Waamini wanapenda kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha kutoka katika undani wa mioyo yao kwa kuwaacha maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni peke yao katika shida na mahangaiko yao. Hapa waamini wanataka sasa kuwa na mwamko mpya wa kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya mafao na ustawi wa jirani zao. Ni mwaliko wa kuwa kweli ni watu wa Kiekaristi.

Waamini wanaomba msamaha kwa vijana kwa kutowasaidia kutimiza ndoto zao, sasa Jimbo linataka kutoa kipaumbele cha pekee katika majiundo awali na endelevu kwa vijana ili waweze kuwa kuweli ni washiriki wakuu katika Uinjilishaji Mpya. Kanisa linataka kuwajengea vijana na watoto uwezo kwa njia ya elimu. Ni hija ya kuomba msamaha kwa wasio amini, ili kuanza mchakato wa majadiliano, ili hatimaye, waweze kuonja utamu wa kukutana na Yesu Kristo mkombozi wa ulimwengu.

Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko jimboni humo ni changamoto ya kuangalia mikakati ya kichungaji kadiri ya vipaumbele vinavyoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi: ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, utu na heshima ya binadamu, mshikamano na upendo kwa kukazia mambo msingi katika maisha. Ni fursa ya kuondokana na ubinafsi. Hija ya Baba Mtakatifu ni changamoto makini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu.
All the contents on this site are copyrighted ©.