2014-06-20 11:44:55

Mshikamano wa upendo na wahamiaji kutoka Kaskazini mwa Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kaskazini, CERNA katika mkutano wake wa mwaka uliofanyika mjini Roma hivi karibuni linasema kwamba, litaendelea kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Kaskazini mwa Afrika, lakini kamwe halitasita kukemea nyanyaso na dhuluma wanazotendewa wakimbizi na wahamiaji hawa sehemu mbali mbali za dunia.

Maaskofu katika mkutano wao wamejadili pamoja na mambo mengine ujasiri, matumaini na imani inayoshuhudiwa na wakimbizi pamoja na wahamiaji katika Jumuiya zile ambazo wanapokelewa kwa heshima na tahadhima, kiasi kwamba wanakuwa ni chachu ya maisha mapya. Maaskofu wanasikitishwa na mambo ambayo yanapelekea kwa wananchi wengi kutoka Kaskazini mwa Afrika kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta nafuuu ya maisha ughaibuni ambako wengi wao wanateseka sana.

Kuna baadhi ya watu ambao wananyanyaswa, utu na heshima yao havithaminiwi, kiasi cha kujikuta wanatumbukia katika biashara haramu ya binadamu au kuchukuliwa kuwa wahuni na watu wasiotakikana katika jamii, kumbe kimsingi ni watu waliokuwa na heshima zao huko wanako toka! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa na watu wenye mapenzi mema kuwa makini dhidi ya biashara haramu ya binadamu inayoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Kuna wanawake na watoto ambao wametumbukizwa katika utumwa mamboleo.

Wakimbizi na wahamiaji wanaofika Kaskazini kwa Afrika kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wanapaswa kupokelewa na kutunzwa kwa heshima na wala wasifikiriwe kwamba ni "wageni wa kuja na kupita" kama ilivyobainishwa huko Morocco. Hapa kuna haja ya kuwa na mikakati makini ya kuwapokea na kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Maaskofu kutoka Afrika ya Kaskazini wanawashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika pamoja na kusaidia mchakato wa taasisi zinazowapokea kuzingatia sheria za kimataifa pamoja na haki msingi za binadamu.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika limepembua pia hali halisi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi inayoendelea kujitokeza katika Nchi za Afrika ya Kaskazini na athari zake katika maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Maaskofu wanasema, kumekuwepo na mfumuko mkubwa wa familia kutengana kutokana na vishawishi vya maendeleo na mambo ya ulimwengu, jambo ambalo linatishia ustawi na mshikamano wa kifamilia.

Kuna idadi kubwa ya wanafunzi wanaotoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaotafuta nafasi za masomo na majiundo makini Kaskazini mwa Afrika, jambo ambalo linahitaji kweli kuwa na mshikamano wa mikakati na shughuli za kichungaji kimataifa, ili kuwasaidia wanafunzi hawa kufikia lengo lao msingi, yaani kupata elimu, ujuzi na maarifa, vinginevyo wanaweza kujikuta wametumbukia kwenye genge la walanguzi na wahuni. Hii ni changamoto kwa wadau mbali mbali kutoa taswira kamili ya Kanisa la Kristo Kaskazini mwa Afrika.

Kutokana na changamoto hiz, CERNA inaandaa Waraka wa pamoja utakuwa kugusia kuhusu wajibu wao wa kuwa ni wahudumu wa fadhila ya matumaini na kwamba, wanatarajia kuiwasilisha kwa Baba Mtakatifu ifikapo mwaka 2015, wakati wakatapokuwa wanafanya hija yao ya kitume inayofanyika kila baada ya miaka mitano mjini Vatican. Maaskofu wakati wa mkutano wao hapa mjini Roma, wamebahatika pia kushiriki katika Ibada za Misa Takatifu zilizokuwa zinaendeshwa na Baba Mtakatifu, wakashuhudia unyenyekevu na changamoto zake kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo.

Maaskofu kutoka Kaskazini mwa Afrika wameangalia pia kuhusu maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu Familia yatakayoanza kutimua vumbi mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba, 2014. Waamini wengi kutoka Kaskazini mwa Afrika wanaishi katika ndoa mseto, changamoto ya kutafuta mbinu na mikakati ya kuziwezesha familia hizi kuendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake wa malezi na majiundo kwa watoto wao.

Maaskofu wamekazia pia umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene Kaskazini mwa Afrika, kwa kutambua kwamba hii ni changamoto kubwa na kadiri inavyokuwa ngumu hivyo ndivyo inavyowawajibisha kuendelea kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. Kuna haja pia ya kuratibu shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika kwa kushirikiana na wadau wengine kwani hii ni dhamana nyeti, peke yao inaweza kuwaelemea na hivyo kushindwa kuitekeleza barabara.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika, limeonesha wasi wasi wake kutokana na ghasia pamoja na kinzani za kijamii zinazoendelea kujitokeza nchini Lybia, kiasi kwamba, baadhi ya viongozi wa Kanisa kutoka Lybia wameshindwa kutoka nchini humo kwa sababu za kiusalama. Mkutano wa CERNA utafanyika tena hapo tarehe 8 Mei 2015 mjini Roma wakati wa hija za kitume mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, CERNA inaunganisha nchi za Algeria, Lybia, Tunisia na Morocco.All the contents on this site are copyrighted ©.