2014-06-20 08:16:43

Kumbu kumbu ya Mtaguso wa NICEA kufanyika mwaka 2025


Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalem, limekuwa ni tukio ambalo limeamsha tena hisia za kuendeleza majadiliano ya kiekumene kati yake na Patriki Bartolomeo wa kwanza wa Costantinopoli. RealAudioMP3

Viongozi hawa wawili wanaendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuponya madonda ya utengano miongoni mwa Wakristo. Panapo majaliwa, viongozi hawa wamepanga tena kukutana na kusali pamoja kunako mwaka 2025, kama kumbu kumbu ya Mtaguso wa Nicea uliofanyika kunako mwaka 325, yapata karne kumi na saba zilizopita. Hii ilikuwa ni Sinodi ya kiekumene iliyoandika Kanuni ya Imani anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakati akizungumza na Shirika la Habari la Asia News.

Mtaguso wa Nicea uliofanyika kunako mwaka 325 uliwakusanya Maaskofu 300 kutoka Makanisa ya Mashariki na Magharibi na hapo wakaandika Kanuni ya Imani inayoendelea kutumika hadi leo hii katika Ibadan a Liturujia mbali mbali za Kanisa. Hii ni mipango ya muda mrefu ili kuganga na kuponya madonda ya utengano miongoni mwa Wakristo. Kwa wakati huu viongozi hawa wawili wanaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika kuimarisha na kukuza urafiki na ushirikiano wa kiekumene baina ya Makanisa haya mawili.

Akizungumzia kuhusu mkutano huu, Professa R. Andrew Chesnut kutoka Chuo Kikuu cha Commonweath anasema, tukio hili si tu kwa ajili ya kuendelea kuboresha mahusiano ya kiekumene baina ya Makanisa haya mawili, bali pia unalenga zaidi kuunga mkono Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya kati.

Viongozi hawa wawili wamekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuwatetea Wakristo wanaoteseka na kudhulumiwa huko Mashariki ya Kati na kwamba, idadi ya waamini wa Makanisa haya inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na madhulumu ya kidini.
All the contents on this site are copyrighted ©.