2014-06-20 14:01:27

Dawa za kulevya ni haramu!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 20 Juni 2014 amekutana na wajumbe waliokuwa wanashiriki kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu uthibiti wa dawa za kulevya, tatizo ambalo linaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu wa nyakati hizi.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mkutano wao utazaa matunda yanayokusudiwa lakini zaidi kwa kufikia malengo waliyojiwekea wakati wa mkutano huu uliokuwa unafanyika mjini Roma yaani: kuratibu sera za kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kushirikishana habari pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaotumika kwa ajili ya kudhibiti biashara haramu ya dawa za kulevya.

Baba Mtakatifu anasema biashara haramu ya dawa za kulevya ni janga ambalo linaendelea kukua na kukomaa siku hadi siku, kiasi cha kuvuka mipaka na jiografia za kitaifa hadi kufikia ngazi ya kimataifa, kiasi cha kuhatarisha maisha ya vijana. Kutokana na hali hii, Baba Mtakatifu anasema anapenda kuonesha wasi wasi na masikitiko yake makuu.

Jamii haiwezi kushinda vita dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa kuruhusu matumizi ya dawa hizi; wala kuponya magonjwa kwa dawa za kulevya. Hapa kuna haja ya kusema wazi kwamba, hakuna sababu ya msingi ya kuruhusu matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwa kuonesha upendo kwa zawadi ya uhai pamoja na kuwashirikisha wengine upendo.

Ni changamoto ya kujikita katika kuwafunda vijana madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya; kutengeneza fursa za ajira pamoja na kuwekeza katika uzalishaji ili watu waweze kupata ajira. Hakuna nafasi kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia na wala kuunda utegemezi kwa mambo mengine yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu anasema Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwahudumia watu katika mahangaiko yao ya ndani, kwa kuwatibu wagonjwa, kuwalisha wenye njaa na kuwatembelea wafungwa. Kanisa halitawaacha pweke wale waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, atawasaidia ili waweze kutambua tena utu na heshima yao, kwa kugundua rasilimali na karama zilizokuwa zimefunikwa na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Vijana waliochakachua maisha yao kwa kubwia dawa za kulevya, waanze mchakato wa kuboresha tena maisha yao, kwa kuwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.All the contents on this site are copyrighted ©.