Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amewataka wananchi
wote wa Kenya kushikamana kwa pamoja ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano
wa kitaifa, ili kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho na kwamba, sera za
kikabila na kidini zinazotaka kuwagawa wananchi wa Kenya hazina mashiko wala ustawi
kwa maendeleo ya wananchi wa Kenya.
Ni dhamana na wajibu wa viongozi wa kisiasa
nchini Kenya kuonesha ukomavu wao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora unaoshuhudiwa
kwa njia ya maisha na maneno yao wanapokuwa jukwaani. Kila mtu anapaswa kusimama kidete
kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kwa njia hii wananchi wa Kenya wanaweza kujenga mazingira ya kuheshimiana na kuthaminiana
kama ndugu.
Kardinali John Njue ameyasema haya hivi karibuni wakati alipokuwa
anatoa tuzo kwa wanamichezo bora walioshiriki katika michezo kwa ajili ya kukusanya
fedha ili kusaidia mchakato wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Kardinali Maurice Otunga
kuwa Mwenyeheri na hatimaye, Mtakatifu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mchakato kwa ngazi
ya Kijimbo, ulioanza Novemba 2011 ulikamilika mwaka 2013 na sasa umepelekwa mjini
Vatican kwa tathmini ya kina.
Ni matumaini ya Kardinali John Njue kwamba,
Mtumishi wa Mungu Kardinali Otunga atakuwa ni Mkenya wa kwanza kuandikwa katika Orodha
ya Watakatifu ndani ya Kanisa Katoliki.