2014-06-19 08:15:46

Tafuteni mafao ya wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada hivi karibuni limemwandikia barua Waziri mkuu wa Canada Bwana Stephen Harper kumtaka kusimamia kwa dhati kabisa sera na mikakati ya kisiasa inayojikita katika kutafuta mafao ya wengi na kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapendi ya Mungu. RealAudioMP3

Wanasiasa wanapaswa kuwa mwelekeo mpana katika utekelezaji wa majukumu yao si tu nchini Canada bali pia kwa kuangalia ustawi na maendeleo ya dunia inayowazunguka.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasikitika kusema kwamba majadiliano ya kisiasa yanayoendelea nchini humo kuhusu utakatifu wa maisha, hususan mtoto anapotingwa mimba tumboni mwa mama yake na mwisho wa maisha ya mwanadamu ni mambo ambayo hayaendi sawasawa, kwani wanasiasa wanataka kuweka rehani zawadi ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Hali hii inadhalilisha utu na heshima ya binadamu, jambo ambalo haliwezi kukubalika kamwe!

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kwa mtazamo mpana linajaribu kupembua hali ya kiuchumi sehemu mbali mbali za dunia kwa kusema kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinaendelea kuwatendea watu wengi duniani kwa kukosa fursa za ajira na hivyo kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa familia na jamii husika.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni mzigo mkubwa kwa nchi zinazoendelea duniani kiasi kwamba watu wengi wanaendelea kutumbukizwa katika lindi la umaskini au kulazimika kuzikimbia nchi zao na matokeo yake, watu wengi wanaendelea kupoteza maisha kwa kufa maji baharini au jangwani kabla ya kufikia ndoto zao za maisha bora zaidi. Vita na ukosefu wa amani na usalama ni mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuyashughulikia kwa kina na mapana, vinginevyo dunia hii itaendelea kuwa ni uwanja wa fujo, ikitawaliwa na falsafa ya “mwenye nguvu mpishe”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakumbuka mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka ishirini iliyopita; vita inayoendelea kupukutisha maisha ya watu nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Sudan ya Kusini bila kusahau vitendo vya kigaidi ambavyo vinaendelea kuitikisa Nigeria na sehemu nyingine za Bara la Afrika. Kuna kundi kubwa la watu ambalo limetekwa nyara huko Nigeria na Cameroon. Yote haya ni matukio yanayohitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kupata suluhu ya kudumu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaishukuru Serikali kwa msaada wake wa hali na mali kwa ajili ya wananchi wa Syria wanaoteseka kutokana na vita pamoja na mikakati ya Serikali katika kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu huko Mashariki ya Kati. Wanaiomba Serikali kuendelea kufanya maboresho katika sheria za uhamiaji pamoja na kusaidia mchakato wa upatikanaji wa amani nchini Venezuela.

Katika masuala ya kimataifa, Maaskofu wanaendelea kukazia umuhimu wa kujikita katika mchakato wa kidiplomasia na majadiliano yanayojikita katika ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi. Vita na matumizi ya nguvu ni sera ambazo zimepitwa na wakati n ani chanzo kikuu cha maafa na kikwazo cha maendeleo ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika kuheshimu na kuthamini utu wa mwanadamu, ili kukoleza haki na amani mambo muhimu sana katika ujenzi wa jamii yoyote ile!

Imeandaliwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.