Askofu Benjamin Ndiaye, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu kutoka Senegal,
Mauritania, Cape Verde na Guinea Bissau amewataka wananchi wa Senegal kutouza kura
zao kwa wanasiasa walaghai wanaotaka kujinufaisha wao wenyewe, bali wahakikishe kwamba,
wanatumia kura yao vyema kama sehemu ya mchakato wa kushiriki katika ujenzi wa nchi
yao. Kila mtu achague kiongozi anayemtaka kwa kufuata dhamiri yake nyofu na kamwe
wasikubali kununulia kwama bidhaa sokoni na hivyo kupoteza uhuru wao kidemokrasia!
Askofu
Ndiaye anawataka pia wanasiasa wanaojiandaa kushiriki kwenye kinyang'anyiro cha madaraka
wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Senegal Jumapili tarehe 29 Juni
2014 kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa; daima walenge kusimamia
kidete mafao ya wengi, ili hatimaye, waweze kuleta mabadiliko makubwa yanayotarajiwa
na wananchi wengi wa Senegal.
Halmashauri ya Walei Jimbo kuu la Dakar, Senegal
linawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kwa kikamilifu pamoja
na kuhakikisha kwamba, uchaguzi unaendeshwa kwa misingi ya ukweli, uhuru na haki.
Uchaguzi mkuu uliopita nchini Senegal, uliacha kurasa chungu na za majonzi kwa wananchi
wengi, jambo hili lisijirudie tena, kwa viongozi wa kisiasa na mashabiki wao kuendesha
kampeni za kitastaarabu, zinazoheshimu na kuzingatia utawala wa sheria, ushindani
wa nguvu ya hoja na mikakati thabiti ya maendeleo ya watu. Lengo ni kuunda Serikali
ambayo itajikita katika mchakato wa kuendeleza mafao ya wengi na maendeleo endelevu
ya wananchi wa Senegal.