Askofu Emmanuel Barbara, wa Jimbo la Malindi na msimamizi wa kitume Jimbo kuu la Mombasa,
Kenya amewataka waamini na wananchi wanaoishi kwenye Ukanda wa Pwani kuwa macho na
watu wanaotaka kuchafua misingi ya haki, amani na utulivu kutokana na kukithiri kwa
mashambulizi ya kigaidi ambayo yanaendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na
hatia.
Vitendo vya kigaidi vinaendelea kusababisha hofu na maafa makubwa kwa
wananchi wa Kenya. Mauaji ya watu kwa misingi ya kidini ni dhana chafu sana inayoweza
kusababisha kinzani na migogoro ya kidini isiyokuwa na mashiko wala tija anasema Askofu
Barbara wa Jimbo Katoliki la Malindi. Mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa kwenye
kitongoji cha Mpeketoni yalikuwa yameandaliwa kwa ufundi mkubwa.
Kinzani na
migogoro ya kisiasa kati ya Serikali na Vyama vya upinzani ni cheche ambazo zinaweza
kupelekea ukosefu wa amani na utulivu nchini Kenya. Askofu Barbara anawataka wananchi
wote wa Kenya kushinda kishawishi ya kugubikwa kwa chuki, uhasama na moyo wa kutaka
kulipizana kisasi!