Changamoto ya kusimama kidete kutangaza Injili ya Uhai na Utamaduni wa amani!
Makatibu wakuu kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE
wameanza mkutano wao wa arobaini na mbili unaofanyika mjini Strasburg, Ufaransa kuanzia
tarehe 19 hadi tarehe 22 Juni 2014, kwa pamoja wakidhamiria kusimama kidete kuendeleza
Injili ya Uhai na Utamaduni wa Amani. Baraza la Jumuiya ya Ulaya lina mchango mkubwa
katika maamuzi mazito kwa wananchi wa Ulaya katika masuala ya kijamii na kitamaduni.
Mkutano huu unalenga kuwasaidia Makatibu wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu kufahamu
kwa kina na mapana mchango unaotolewa na Baraza la Ulaya katika masuala ya kidemokrasia,
haki msingi za binadamu, amani na maendeleo endelevu ya binadamu: Uhai wa binadamu
na uhuru wa kuabudu ni kati ya mambo ambayo ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume
wa Kanisa, kumbe ni masuala ambayo yanapaswa kuangaliwa na kupewa uzito unaostahili
kutoka kwa Baraza la Jumuiya ya Ulaya na Makanisa Barani Ulaya.
Itakumbukwa
kwamba, Baraza la Umoja wa Ulaya linaundwa na nchi wanachama 47 zinazowakilishwa pia
kwenye Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya. Ni Jumuiya ambayo
inahistoria tofauti na kwa baadhi ya nchi historia yake imechafuliwa kwa damu ya watu
wasiokuwa na hatia, lakini Jumuiya ya Ulaya ina mizizi na chimbuko lake katika tunu
msingi za maisha ya Kikristo, historia ambayo ina zaidi ya miaka elfu mbili! Mkutano
huu unafanyika kwa faragha!