2014-06-19 09:29:22

Caritas Mbeya inawashukuru wafadhili katika mapambano dhidi ya Ukimwi!


Hivi karibuni mkurugenzi wa Global Health program kutoka nchini Marekani, Bwana Tiffany Hamm kwa kushirikiana na shirika la water Reed/HJFMRI imeipongeza Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya kwa juhudi zake za ari na mali za kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi katika jamii kwa shirikiana na serikali ya Tanzania.

Mkurugenzi huyo aliongozana na ujumbe wa wafanyakazi wenzake watano kutoka nchini Marekani ambao ni Sundha Srinagesh Mkurugenzi katika ofisi inayoshughulikia masuala ya ufadhili, Meneja kutoka timu inayoshughulikia mikataba HJMRI Troy Hagrove na Meneja program Eric Black.

Wengine ni pamoja na wafanyakazi wa Water Reed/HJFMRI kutoka makao makuu ya Tanzania yaliyopo mkoani Mbeya wakiongozwa na Mkurugenzi wa tanzania Klaus Sturbeck ambapo pamoja na mambo mengine wametembelea kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya kuhusu masuala ya vita dhiti ya maambukizi ya ukimwi na ukimwi, Ukatili wa kijinsia, ukatili kwa watoto pamoja na Saratani ya uzazi.

Tiffany amesema mashirika mengine yanapaswa kuiga mfano wa Idara ya Caritas Mbeya kwa kufanyakazi wa kujitoa kwa moyo wao wote na kwa nguvu zao zote kwa kushirikiana na jamii pamoja na serikali jambo ambalo linaleta matumaini makubwa kwa watu wenye shida mbalimbali za kiafya hususani maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi na saratani ya shingo ya kizazi.

Licha ya kuwepo kwa jitihada za dhati za serikali kushirikiana na wafadhili kutoka nchi mbalimbali kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na Ukimwi, bado kumekuwepo na changamoto ambazo zinachelewesha harakati hizo ikiwemo umaskini,imani za kidini, mila na desturi sanjari na watendaji wasio waaminifu na wasiozingatia maadili ya kazi.

Mwenyekiti wa mtaa wa Nkuyu, Kata ya Iganzo jijini Mbeya, Peter Mwamwaja akijibu swali lililoulizwa na Mkurugenzi wa Shirika la Water Reed-Tanzania, Klaus Sturbeck ametaja mojawapo ya changamoto wanayokumbana nayo kuwa ni baadhi ya watu wanaojikuta wakiwa na maambukizi baada ya kupima kujisikia vibaya na hatimaye kukimbia kwa kuhama mtaa mmoja na kukimbilia mwingine.

"Watu wanaona aibu wakishapima na kupata majibu na wakijikuta wameambukizwa wanaondoka Iganzo na kuhamia pengine Kata ya mwakibete,huko wanajificha na kuendeleza ngono na matokeo yake maambukizi yanazidi kuongezeka, tunajitahidi kuwashauri na kuwashirikisha wahudumu wa Caritas na tunafanikiwa,"anasema Mwenyekiti huyo.

Msimamizi wa huduma majumbani, Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya Upendo Mwaipopo naye anasema umaskini kwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi na kujikuta wakipisha siku bila kula ni mojawapo ya sababu inayowafanya baadhi yao kuacha kutumia dawa wakidai zinawatesa tumboni na kuwamaliza nguvu. Ofisa afya ya jamii Kata ya Iganzo, Asteria Kayange anaelezea namna anavyopambana na changamoto ya waathirika kujinyanyapaa baada ya kubaini wanaishi na maambukizi kwa kujenga mazoea ya kuwa nao jirani na kuwashauri kujikubali.

Mtendaji wa mtaa wa Nkuyu na Mwambenja, Mage Makwenda akifafanua swali lililoulizwa na ujumbe huo endapo anaifahamu idara ya Caritas na maendeleo Jimbo katoliki la Mbeya na baadhi ya wahudumu wake anasema wamekuwa wakifanyakazi kwa pamoja na mawasiliano muda wote na amepongeza kwa wepesi wao wa kufika pindi wanapohitajika kwa haraka.

Suala la mfumo dume katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi bado imekuwa ni changamoto kubwa kama ambavyo Mweka hazina wa kikundi cha watu wanoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi cha Wemavinga, Kata ya Iganzo, Pendo Machonga anavyosema kuwa suala la kupima afya ni na kila mmoja wetu na kuwataka wanaume kuacha tabia ya kuwatumia wanawake kama kioo cha kujitazamia majibu ya afya zao.

Mratibu wa kitengo cha Ukimwi, jinsia, wanawake na watoto ,Idara ya Caritas Jimbo Katoliki la Mbeya Praxeda Manyuka amelishukuru Shirika la Water reed/HJFMRI na wafadhili wengine kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuunga mkono harakati za kupambana na maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Saratani ya kizazi, ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Caritas na maendeleo Jimbo Katoliki la Mbeya, Anthony Kisengo kwa niaba ya Mkurugenzi Edgar Mangasila amesema kwa niaba ya Askofu Evaristus Marcus Chengula (IMC) anapenda kuwapongeza na kuwaomba waendelea kusaidiana katika kuikomboa jamii. Mmoja wa viongozi wa kikundi cha uhamasishaji cha vijana klabu kinachohudumiwa na Caritas Mbeya, Brown Isaya ametoa wito kwa serikali na wadau wengine kuwasaidia kwa ari na mali ili waweze kufanikisha lengo la kutoa hamasa kwa jamii kuhusu mapambano ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi.

Na Thompson Mpanji,
Mbeya, Tanzania.
All the contents on this site are copyrighted ©.