Askofu mkuu Luigi Travaglino, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya
Umoja wa Mataifa yenye makao makuu yake mjini Roma, hivi karibuni alishiriki katika
mkutano wa thelathini na mbili wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa,
FAO kwa ajili ya Ukanda Amerika ya Kusini na Caraibi kwa kusema kuna haja ya kutoa
majibu makini kwa watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani.
Baba Mtakatifu
Francisko anasikitika kusema kwamba, hata katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi,
teknolojia, uzalishaji na tija, bado kuna watu wanakufa kwa baa la njaa duniani wakati
sehemu nyingine za dunia, watu wanaendelea kushiba na kusaza, jambo ambalo halikubaliki
kamwe.
Kuna chakula cha kutosha kuweaza kuganga baa la njaa, shida ni mgawanyo
wa chakula hiki, changamoto ya kutoa mwelekeo wa kiutu zaidi kuliko kung’angania tu
mwelekeo wa teknolojia katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Jumuiya
ya Kimataifa haina budi kujikita katika uhakika wa usalama wa chakula duniani, kwa
kuzalisha chakula cha kutosha pamoja na kuboresha ugavi wake.
Juhudi hizi
hazina budi kwenda sanjari na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato unaoendelea
kuwaandama watu wengi duniani pamoja na kuendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana
katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa Mwaka 2015, katika mchakato wa kupunguza
kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na utapimlo mkali
duniani.
Mikakati ya mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini, inakwamishwa
kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yameendelea kuwa ni chanzo kikuu
cha maafa sehemu mbali mbali za dunia. Sera tenge katika masuala ya uzalishaji, ugavi
na masoko zimepelekea baadhi ya watu kunyimwa fursa ya kuuza mazao yao kwenye soko
la pamoja, hali ambayo inazilazimisha baadhi ya nchi kuendelea kuagiza chakula cha
msaada kutoka nje ya nchi zao! Ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana
ni jambo linalochangia kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa Jamii.
Mbinu mkakati
wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula hauna budi kulenga zaidi katika uzalishaji
wa mazao ya chakula vijijini, kwa kuzingatia wingi na ubora pamoja na kuwajengea uwezo
wakulima wadogo wadogo kwa njia ya vyama vya ushirika. Mwaka wa Kimataifa wa Wakulima
Vijijini unaoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa, uliopendekezwa na Shirika la Kilimo
na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, usaidie kuweka mikakati makini ya shughuli za
kilimo vijijini, kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu.
Askofu mkuu Luigi
Travaglino anasema kwamba, Familia za wakulima vijijini, zikijengewa uwezo, zinaweza
kushiriki vyema zaidi katika kulinda na kutunza mazingira kwani kazi na familia ni
kama chanda na pete katika kudumisha misingi ya upendo, umoja na udugu kati ya watu
pamoja na kuwasaidia wanyonge. Mageuzi ya kilimo yanayozingatia maendeleo ya kweli
ya binadamu ni jambo la msingi. Wananchi wahusishwe kikamilifu katika ulinzi na usimamizi
wa mazingira, kwani mipango na mikakati ya maendeleo isiyotoa kipaumbele cha kwanza
kwa binadamu na mahitaji yake haina tija wala mashiko kwa maendeleo ya watu!
Mapambano
dhidi ya baa la njaa yataweza kupata mafanikio makubwa, ikiwa kama wakulima, serikali,
mashirika ya kimataifa, vyama vya kiraia, vyama vya ushirika na wawekezaji binafsi
katika sekta ya kilimo watashirikishwa kikamilifu, ili kujenga na kuimarisha uchumi
jamii unaokidhi mahitaji ya watu! Ili kufanikisha azma hii kanuni maadili ya mshikamano
inapaswa kutekelezwa. Hii ni kanuni inayopewa msukumo wa pekee na Kanisa katika Mafundisho
yake Jamii.
Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu wa Kanda ya Amerika ya Kusini
na Caraibi, umeipongeza FAO kwa kuendelea kushirikiana na Serikali mbali mbali katika
mchakato wa kupambana na baa la njaa duniani. Vatican itaendelea kushirikisha mchango
wake katika masuala ya kimaadili ili kuwa na siasa na sera makini za maendeleo zinazotoa
kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu, utu na maendeleo yake endelevu!
Imeandaliwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.