2014-06-18 08:20:14

Liturujia na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika Liturujia kwa kutambua nafasi ya Liturujia katika Fumbo la Kanisa, kwani Liturujia ni kilele na chemchemi ya maisha ya Kanisa. Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi makini ya Kiliturujia pamoja na ushiriki hai wa waamini. RealAudioMP3

Ni Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican walitambua na kuthamini umuhimu wa kutafsiri vitabu vya Liturujia ili Ibada mbali mbali ziweze kufahamika na wengi: kwa kukazia ukamilifu na ufahamu wa Ibada inayoadhimishwa. Liturujia irekebishwe kulingana na hali za watu na Mapokeo yao, kwa maneno mengine, huu ulikuwa ni mwanzo wa jitihada za utamadunisho wa Liturujia katika uhalisia wa maisha ya waamini sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali George Pell, hivi karibuni alipokuwa anachangia kwenye Kongamano la Liturujia, Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu Liturujia ya Kanisa, Sacrosanctum Concilium, SC, alisema, Papa Paulo VI alikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kutafsiri kwa uaminifu vitabu vya Liturujia ya Kanisa, kwani hii ni sauti ya Kanisa. Lugha inayotumika inapaswa kueleweka na hadhira inayokusudiwa pamoja na kuwakilisha Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa.

Hii ni lugha ya kawaida inayotumiwa na watu ili upendo wa Mungu uweze kugusa akili na mioyo ya watu wakati wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Wale waliopewa dhamana ya kutafsiri vitabu vya Liturujia ya Kanisa wanatekeleza dhamana na utume wa Maaskofu mahalia wa kufundisha, kumbe, wanapaswa kuitekeleza kazi hii kwa ari na moyo mkuu, wakiendelea kuwa waaminifu kwa Maandiko Matakatifu.

Kutokana na mwamko uliokuwa umeletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Biblia iliweza kutafsiriwa katika lugha mbali mbali kuanzia miaka 1966 kwa kutumia lugha inayoeleweka kwa watu wa nyakati hizi. Kardinali George Pell anasema, Biblia nyingi ziliuzwa wakati huo, kwa lengo la kutaka kusambaza Habari Njema ya Wokovu kwa Wakristo waliokuwa wanaishi Barani Afrika na Asia. Ilikuwa ni lugha iliyoeleweka hata miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Huu ukawa ni mwanzo wa mchakato wa kuwajengea uwezo waamini wa Kanisa Katoliki kupenda kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Itakumbukwa kwamba, kabla ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican Biblia Takatifu ilikuwa inamilikiwa na Mapadre na Watawa, waliokuwa na uwezo wa kusoma na kufahamu yale yaliyokuwa yameandikwa.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliendelea kukazia kwamba, Kanisa lilikuwa na dhamana ya kuhakikisha kwamba, linasambaza Biblia kwa kuwa na tafsiri sahihi, ili neema na baraka za Kristo ziweze kuwafikia waamini kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Biblia Takatifu ni urithi mkubwa kutoka katika Kanisa la mwanzo, kazi iliyofanywa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na hatimaye, Kanisa likakubaliana na Vitabu ambavyo vitaingizwa katika Biblia Takatifu.

Hakuna uhusiano wowote kati ya tafsiri ya Biblia na Kanisa Katoliki anasema Kardinali George Pell, lakini Kanisa lilikuwa na dhamana na wajibu wa kutoa tafsiri sahihi ya Neno la Mungu kwa ajili ya ustawi wa roho za waamini wake. Ndiyo maana tafsiri zilizofanywa na Makanisa mahalia zilipaswa kupata kibali kutoka Vatican kabla ya kuanza kutumika. Bado kuna haja ya kuwa waaminifu katika kufanya tafsiri ya vitabu vya Liturujia ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.