Kardinali Pengo aweka jiwe la msingi la Chuo Kikuu MUCO Bagamoyo!
Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaendelea kuwekeza kikamilifu katika sekta ya elimu
ili kuwasaidia watanzania kuwa na majiundo kamili ili kukabiliana barabara na changamoto
za maisha, ili hatimaye, Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Shirika
la Roho Mtakatifu ambalo kwa miaka mingi limewekeza na kuona mafanikio makubwa katika
sekta ya elimu nchini Tanzania, sasa limeanza kujielekeza katika kuanzisha Kitivo
cha Sayansi kitakachokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania,
SAUT. Kitivo hiki kitajulikana kama “Marian University College”, kwa kifupi MUCO,
ambacho kinajengwa kwenye mji mkongwe wa Bagamoyo, Mkoani Pwani, nchini Tanzania.
Hivi
karibuni, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ameweka
jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo kikuu cha MUCO na kwamba, mwezi Septemba, 2014 kitaanza
kuandikisha wanafunzi, wakati huo huo ujenzi wa majengo mengine ukiendelea kukamilishwa
hatua kwa hatua. Katika hafla ya kuweka jiwe la msingi, Kardinali Pengo amesema, nchi
ambayo haina wataalam wa sayansi, kwa hakika itachechemea katika ushindani wa maendeleo
na mataifa mengine. Umefika wakati kwa watanzania kujiekeza zaidi katika masuala ya
kisayansi ili kupata maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho
na kimwili.
Akizungumza katika tukio hili Padre Florentin Mallya, Makamu mkuu
wa Shirika la Roho Mtakatifu Afrika Mashariki amesema, MUCO itaendelea kushirikiana
na SAUT, hadi pale mchakato wa kukiwezesha Chuo kikuu cha MUCO kujitegemea na kuwa
Chuo kikuu kamili. Kuanzishwa kwa MUCO ni kujibu kwa dhati changamoto inayotolewa
na Serikali ya Tanzania kwa sekta binafsi kusaidia mchakato wa kukuza na kuendeleza
sekta ya elimu hususan katika mchepuo wa sayansi, ili kujibu mahitaji makubwa yanayoendelea
kujitokeza ndani na nje ya Tanzania katika masuala ya elimu.
Huu ni mwendelezo
wa huduma ya elimu inayotolewa na Shirika hili katika shule zake za awali na sekondari
ambazo kwa miaka mingi zimeendelea kupeta nchini Tanzania kutokana na wanafunzi wanaohitimu
katika shule hizi kuwa na kiwango kikubwa cha ufaulu kwenye mitihani. Wazazi waliokuwa
wanahaha kuwatafutia watoto wao mahali pazuri zaidi pa kusoma, sasa MUCO itakuwa ni
jibu lao makini.
Ni kutokana na changamoto zote hizi, Shirika la Roho Mtakatifu
liliomba ushirikiano na Serikali ya Tanzania ili kutekeleza azma hii kwa ajili ya
ustawi na maendeleo ya watanzania tangu shule za msingi hadi chuo kikuu. Shirika
linapania kuendelea kutoa kiwango bora cha elimu kwa kutambua kwamba, hii ni sehemu
ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Shirika
linaiomba Serikali ya Tanzania pamoja na wazazi kuendelea kuonesha mshikamano katika
kufanikisha malengo ya maboresho ya elimu nchini Tanzania.