2014-06-18 11:22:42

Injili ya Familia kutoka Barani Afrika!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Benin, hivi karibuni limehitimisha warsha ya siku tatu kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 5 hadi 19 Oktoba, 2014 mjini Vatican.

Warsha hii imepembua pamoja na mambo mengine furaha, changamoto na matatizo yanayozikabili familia za Kiafrika katika mchakato wa kutangaza Injili ya Familia mintarafu dhamana ya Uinjilishaji Mpya. Wajumbe wamejiandaa kushirikisha mchango wa Kanisa la Afrika wakati wa maadhimisho haya, kwa kuangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza Barani Afrika, lakini zaidi, Familia ya Mungu Barani Afrika inapenda kushirikisha tunu bora za maisha ya ndoa na familia zinazofumbatwa katika mila na desturi njema za Kiafrika.

Waamini, vyama vya kitume na watu wote wenye mapenzi mema wanaendelea kuhamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo ambao unaonekana kutaka kufifisha Injili ya Familia. Itakumbukwa kwamba, Sinodi ni chombo maalum ambacho Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kwa pamoja kuchambua Injili ya Familia ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati utakaotumiwa na Kanisa katika kujibu changamoto za kichungaji zinazoendelea kujitokeza kwa wakati huu.

Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itaadhimishwa katika awamu kuu mbili: awamu ya kwanza ni Oktoba 2014 na awamu ya Pili itaadhimishwa hapo mwaka 2015, lakini hili ni tukio moja linalopania kuliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja kama Familia ya Mungu inayowajibika.All the contents on this site are copyrighted ©.