Kanisa linaendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Yohane Paulo II katika maisha na
utume wake ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. Ni kiongozi anayekumbukwa kutokana
na mchango wake uliosaidia kuanguka kwa ukomunisti Ulaya Mashariki, miaka ishirini
na mitano iliyopita, tukio ambalo limeleta mabadiliko makubwa na changamoto nyingi.
Kunako mwaka
1989 Mtakatifu Yohane Paulo II alichapisha Waraka unaojulikana kama “Annus Mirabilis”.
Poland kwa mara ya kwanza ikafanya uchaguzi huru na hatimaye, kuanguka kwa Ukomunisti
Ulaya Mashariki.
Hivi karibuni Ubalozi wa Poland mjini Vatican kwa kushirikiana
na Taasisi za Kipapa za Sayansi waliadhimisha tukio hili ambalo liliwashirikisha viongozi
wakuu wa Kanisa kutoka mjini Vatican na Poland. Baadhi ya wadau wakuu katika mageuzi
haya kama vile Lech Walesa, Rais mstaafu wa Poland alitoa ushuhuda wake na kuwataka
wananchi wa Poland kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa siku za usoni, kwa kuzingatia
amri kumi za Mungu, msingi mkuu wa maadili na utu wema.
Jamii haina budi kujikita
katika urithishaji wa tunu msingi za maisha ya kijamii, ili kujenga jamii inayowajibika
na kujikita katika maadili mema. Wadau mbali mbali wametambua mchango uliotolewa na
Kanisa katika kuanguka kwa utawala wa kikomunisti Ulaya Mashariki hata kama Kanisa
liliteseka na kudhulimiwa sana katika nyakati hizi.
Waamini walei kwa njia
ya ushuhuda makini wa maisha yao, walijielekeza zaidi na zaidi katika kuleta mabadiliko,
leo hii Ulaya ya Mashariki licha ya magumu na changamoto nyingi, lakini imeshuhudia
mabadiliko ya kweli, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa mawasiliano. Majadiliano
kati ya watu wasioamini na waamini walei yanayofanyika katika uhalisia wa maisha ni
muhimu sana kama sehemu ya mchakato unaopania kuyatakatifuza malimwengu. Bila kanuni
msingi za maadili na utu wema, dunia inakuwa ni uwanja wa fujo.
Kardinali Paul
Poupard, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, Kanisa lilikuwa mstari
wa mbele kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa kuwajengea watu msingi bora
wa maisha ya kiroho dhidi ya ukanimungu pamoja na kuendelea kuimarishwa kwa mfano
na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyekuwa chemchemi ya imani na matumaini kwa
wananchi wengi wa Ulaya ya Mashariki. Kwa njia hii, watu wengi wakaweza kupata uhuru
wa ndani ambao matunda yake yalijionesha kwa nje katika masuala ya kisiasa na kijamii.
Kardinali
Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali ambaye aliwahi kuwa Katibu mkuu wa Vatican anasema
kwamba, Vatican kuanzia kwenye uongozi wa Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI ilijihusisha
kikamilifu katika kuwajengea watu uwezo wa kujiletea mabadiliko ya kweli katika maisha
yao, kwa kuunga mkono uhuru wa kidini na haki msingi za binadamu. Mambo yote haya
yanaonesha nguvu ya kidini na imani katika mchakato wa kumletea mwanadamu ukombozi
wa kweli. Kwa njia ya nguvu ya imani, mataifa yanaweza pia kupata amani ya kweli kwa
siku za usoni!