Uwekezaji makini usaidie kuleta mabadiliko ya kweli katika Jamii!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Juni 2014 amewashukuru na kuwapongeza
wajumbe wanaohudhuria kongamano la kimataifa linalojadili kwa kina na mapana jinsi
ya kuwekeza ili kuwajengea uwezo maskini katika kukabiliana na mazingira yao sanjari
na kuondokana na ukosefu wa usawa na migawanyiko mikali ya kijamii, kiasi cha kundi
kubwa la watu kuendelea kuogelea katika hali mbaya ya kijamii.
Mwekezaji makini
ni mtu anayetumia rasilimali yake kwa ajili ya kukoleza maendeleo ya maskini kiuchumi
na kijamii, ili kujikwamua kutoka katika mahitaji yao msingi yanayofumbatwa katika
kilimo, maji safi na salama, makazi bora, huduma za elimu na afya. Uwekezaji wa namna
hii unapania kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu, kwa kutengeneza fursa
za ajira, kuwapatia watu nafasi ya kupata huduma ya nishati, elimu pamoja na kuendeleza
mchakato wa maboresho ya tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Matokeo
ya uwekezaji makini yanapimwa kwa mchango wake. Lengo ni kujenga uhusiano wa dhati
kati faida na mshikamano, uwekezaji unaolenga katika majitoleo na maboresho ya maisha
ya watu. Ulimwengu mamboleo una kiu ya kutambua na kuthamini ukweli huu.
Baba
Mtakatifu anasema, sekta ya uchumi na fedha haina budi kuratibiwa na kanuni maadili
na kwamba, soko liwe ni kwa ajili ya huduma ya watu na mafao ya binadamu wote. Ni
jambo lisilovumilika tena kuona kwamba, baadhi ya taasisi za fedha zinaendelea kujitajirisha
badala ya kuhudumia watu katika mahitaji yao msingu au wachache wanaendelea kutajirika
wakati mamillioni ya watu yanatumbukia katika janga la umaskini.
Maendeleo
ya sayansi na teknolojia yanaharakisha mzunguko wa fedha, kumbe kuna haja pia kuboresha
uwezo wa kutoa huduma na kusimamia mafao ya wengi. Upandishaji wa bei ya mazao ya
chakula ni kashfa kubwa inayopelekea watu wengi kukumbwa na baa la njaa duniani. Umefika
wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kukuza soko la uwekezaji utakaokuwa
na mafao kwa jamii, ili kudhibiti uchumi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.
Baba
Mtakatifu anasema, tarehe 16 Juni, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Mashahidi Quirico
na Julitta, Mtoto na Mama, ambao wakati wa madhulumu ya Dioklesiani, waliacha mali
yao yote na kwenda kukabiliana na kifo, mwaliko wa kuchuchumilia mafao ya wengi, kwa
kuonesha upendo na mshikamano kwa maskini na wanyonge ndani ya jamii