Miradi ya maendeleo 125 kwa ajili ya Amerika ya Kusini imepitishwa!
Viongozi wakuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu ambao uko chini ya usimamizi wa Baraza
la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, limehitimisha mkutano
wake wa mwaka uliokuwa unafanyika mjini Vatican kwa kupitisha miradi 125 kwa ajili
ya maendeleo ya wakulima Amerika ya Kusini, kwa gharama ya dolla za kimarekani millioni
1, 8000. 000.
Mkutano huu umefanyika mjini Vatican ili kupata ushauri wa shughuli
za kichungaji kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, wakati huu Mama Kanisa anapojielekeza
zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu
na maendeleo yake kiroho na kimwili. Huu ni mfuko ambao kwa muda wa miaka ishirini
na miwili umekuwa mstari wa mbele katika kuwajengea uwezo wenyeji, ili hatimaye, waweze
kujitegemea na kujiendeleza wenyewe.
Miradi iliyopitishwa kwa mwaka huu inahusu
hasa majiundo makini kwa watoto na vijana Amerika ya Kusini; uchimbaji wa visima vya
maji safi na salama, makazi ya watu pamoja na huduma ya afya.
Baba Mtakatifu
alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu alikazia umuhimu wa
huduma inayotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya maendeleo ya watu na kwamba, hii ni
sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Kanisa halina budi kujielekeza katika
mchakato wa kuwajengea vijana matumaini mapya kwa kuwapatia fursa za ajira pale inapowezekana,
ili kukuza na kudumisha misingi ya maadili na utu wema, vinginevyo vijana hawa wanaweza
kujikuta wakiwa ni wahanga wa vitendo vya kigaidi, mateja ya dawa za kulevya na biashara
haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.
Wajumbe wamebadilishana mawazo na mang'amuzi
yao kuhusu mikakati ya maendeleo, ushirikiano na utekelezaji wa miradi hii kwa ajili
ya mafao na ustawi wa wananchi wa Amerika ya Kusini. Wajumbe wanasema umefika wakati
kwa Mfuko wa Maendeleo ya watu kupanua wigo wake kijiografia, ili kukumbatia upendo
na ukarimu unaooneshwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa watu kutoka sehemu mbali
mbali za dunia. Makanisa mahalia yanaendelea kuhamasishwa kushiriki na kuchangia katika
mikakati ya maendeleo ya watu wao.