2014-06-17 08:28:52

Malawi na maadhimisho ya AMECEA


Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo ndiyo kauli mbiu itakayofanyiwa kazi wakati wa maadhimisho ya mkutano wa 18 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA utakaofanyika, Lilongwe nchini Malawi, kuanzia tarehe 16 – 26 Julai 2014. Mkutano huu ndio ulikuwa ni ajenda kuu ya mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi uliohitimishwa hivi karibuni. RealAudioMP3

Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Familia ya Mungu nchini Malawi kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya mkutano wa AMECEA. Kwa mara ya kwanza AMECEA ilifanya mkutano wake nchini Malawi kunako mwaka 1979 kwa kujielekeza zaidi katika uanzishwaji na uimarishaji wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kama sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji inayofanywana Maaskofu wa AMECEA. Kunako mwaka 1995 Malawi ikawa tena mwenyeji wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa 12 uliofanyika mjini Mangochi kwa kuangalia dhamana ya Kanisa katika maendeleo mintarafu mwanga wa Sinodi ya Afrika.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika mkutano wake limejadili pia kuhusu hija yao ya kitume inayofanyika kila baada ya miaka mitano mjini Vatican kwa kukutana, kusali na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na viongozi waandamizi wa Mashirika ya Kipapa mjini Roma. Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, linatarajia kufanya hija yake ya kitume mjini Vatican kuanzia 6 hadi tarehe 9 Novemba 2014 kadiri ya ratiba iliyotolewa na Sekretarieti ya Vatican.

Maaskofu wamejadili pia kuhusu Chuo Kikuu cha Kikatoliki Malawi; majiundo awali na endelevu ya Makasisi: Katiba ya Chama cha Wakarisimatiki Wakatoliki nchini Malawi; hali ya kisiasa na kijamii wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini humo. Maaskofu pia wamepokea taarifa ya kuhusu Misale ya Waamini kwa lugha ya Chichewa pamoja na taarifa mbali mbali kutoka katika Sektretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi.
All the contents on this site are copyrighted ©.