2014-06-17 15:30:11

Majaji simameni kidete kulinda na kutetea haki; utu na heshima ya binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 17 Juni 2014 amekutana na kuzungumza na Baraza kuu la Majaji nchini Italia kwa kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kudumisha maridhiano ndani ya Jamii. Anawapongeza wote wanaotekeleza dhamana hii wakisukumwa na dhamiri nyofu, kuwajibika barabara kisheria na kiraia.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Majaji amekazia umuhimu wa kujikita katika kanuni maadili, ili kukuza na kudumisha uhuru na ufanisi wa kazi kwa Majaji pamoja na kuendelea kuwa ni watu wasiofungamana na upande wowote; anapima na kuamua katika misingi ya kweli na busara, kwa kujikita katika sheria, dhamiri nyofu na kanuni msingi za maisha. Uhuru wa Jaji na kwa kutoonesha upendeleo ni muhimu katika utekelezaji wa sheria zilizopo. Sheria na madaraka yanapata uwiano wake katika nchi yenye demokrasia katika katika mahakama.

Jaji ni kiongozi anayetegemewa kutoa maamuzi yanayogusa haki, mafao ya raia na wanatarajia pia kupata msaada kutoka kwa Majaji. Kutokana na mahitaji haya, Hakimu katika ngazi yoyote ile ni lazima awe na sifa zifuatazo: mtu mwenye akili, mwenye ukomavu kisaikolojia na maadili mema, mambo yanayomwezesha kuaminiwa anapotekeleza wajibu wake. Lakini Jaji anapaswa kuongozwa na fadhila ya busara, fadhila inayoongoza na kumsukuma kiongoni kutenda kwa haki nje ya mitazamo yake ya ndani, tabia na maelekeo binafsi au siasa.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Majaji kwamba, wananchi wa Italia wanategemea makubwa kutoka kwao kutokana na mabadiliko makubwa yanayojitokeza katika medani za kidemokrasia, kwa kuonesha urithi wa tunu msingi katika maisha. Majaji kamwe wasiwakatishe tamaa wananchi, bali wajitahidi kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kimaadili ndani ya Jamii.

Majaji waendelee kufuata na kuiga mifano ya Majaji waliopeta katika utumishi wao kwa umma. Hawa ni kama vile Jaji Vittorio Bachelet, aliyeongoza Baraza kuu la Majaji nchini Italia katika kipindi kigumu cha historia ya Italia kilichosheheni mauaji ya kutisha. Wengine ni Rosario Livatino, aliyeuwawa na kikundi cha Mafia na sasa yuko kwenye mchakato wa kutangazwa kuwa Mwenyeheri.

Hawa ni watu waliojisadaka na kuonesha ushuhuda wa maisha ya mwamini mlei; watu waliojikita katika majadiliano, wenye ujasiri na waliosimama kidete kulinda na kutetea haki, utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.