Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni tarehe 16 Juni 2014 amefungua Kongamano la
shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma kwa kuonesha umuhimu wa Waraka wa kichungaji
uliotolewa na Mtumishi wa Mungu Paulo VI Evangelii Nuntiandi, Utangazaji wa Injili,
kazi iliyohaririwa kwa ufundi mkubwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.
Katika
hija zake za kichungaji Jimboni Roma Baba Mtakatifu anasema amekutana na watu wenye
imani thabiti na baadhi ya watu wamekata tamaa kutokana na ugumu wa maisha, kiasi
hata cha kupoteza maana ya maisha, changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba,
anawajengea waamini umuhimu wa kuthamini zawadi ya maisha kuanzia katika misingi ya
kifamilia pamoja na kujitahidi kutenga nafasi kwa ajili ya kukaa na familia, ili kuonja
upendo na uwepo wa wazazi ndani ya familia, ili watoto wasijisikie yatima hata kama
wazazi wao bado wako hai!
Baba Mtakatifu anazitaka familia kuonesha moyo wa
sadaka na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume
wa Kanisa. Waamini watambue kwamba, mambo mengi waliyokirimiwa ni neema na zawadi
kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kujisadaka
pia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.
Yesu
amewahakikishia wafuasi wake kwamba, kamwe hatawaacha yatima, hivyo anawaalika kumsikiliza
kwa makini na kuendelea kuwa na matumaini kwake, kwani kamwe hawezi kuwadanganya.
Yesu amewafunuliwa wafuasi wake upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko
kwa waamini kupendana, kuthaminiana na kusaidiana katika hija ya maisha. Kuna idadi
kubwa ya vijana ambao hawana fursa za ajira nchini Italia na Ulaya kwa ujumla, hawa
ni watu wasiokuwa na nafasi, ni watu wanaopuuzwa na kutwezwa. Hii ndiyo taswira ya
jamii ya kiteknolojia isiyojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, jamii ambayo
haina furaha hata kidogo.
Baba Mtakatifu anasema, kupenda na kuthamini zawadi
ya maisha hakuna haja ya kuwa na mambo mengi, bali ni kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa Yesu anayemkirimia mwamini mwelekeo mpya wa maisha unaojikita katika wongofu wa
ndani, ari na mwelekeo wa kimissionari. Wongofu wa ndani ni hija inayohitaji ujasiri
na kuona fadhila ya umama inayojikita katika maisha na utume wa Kanisa; wenye uwezo
wa kuzaa watoto wapya kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.
Yote haya ni matokeo
ya mikakati ya shughuli za kichungaji zinazojielekeza katika Uinjilishaji Mpya. Kanisa
halina budi kujisikia kuwa kweli ni Mama na Mwalimu kwa njia ya mtindo wa maisha na
ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
XVI. Kanisa halina budi kujipyaisha kwa kukazia maisha ya kifamilia na kijumuiya,
mahali ambapo waamini wanakutana na kushirikishana kweli za Kiinjili; mahali ambapo
kweli watu wanajisikia kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu.
Watu wajifunze
kujisadaka kwa kutenga muda kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Kanisa lioneshe
moyo wa upendo kwa njia ya ukarimu kwa wote wanaobisha hodi katika malango yake, hasa
zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu
Francisko anawataka waamini kujenga na kudumisha moyo na utamaduni utakaowawezesha
watu kujisikia kweli wako nyumbani wanapokuwa Kanisani. Anatambua dhamana na majukumu
waliyo nayo Makleri katika utume na kazi za Uinjilishaji. Kashfa na makwazo yaliyotendwa
na baadhi ya Makleri yamekuwa ni chanzo cha baadhi ya watu kutoonekana tena Kanisani,
changamoto ya kujirekebisha na kuanza kweli kutoa ushuhuda wenye matumaini kwa Kanisa
la Kristo.
Watu waonje huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo kwa
njia ya Kanisa lake. Kanisa litafakari, fursa, matatizo na changamoto za vijana, ili
liweze kuwasaidia kukua na kukomaa, ili kweli waweze kuwa ni watu wa matumaini kwa
leo na kesho iliyo bora zaidi. Kanisa liwaonjeshe watu huruma ya Kristo, kwa njia
ya ushuhuda wa maisha ya kila mwamini na wala si kutoka kwa Mapadre, Watawa na Makatekista
au viongozi wa Halmashauri ya waamini walei peke yao.
Ratiba ya shughuli za
kichungaji Parokiani iwawezeshe hata vijana kushiriki kikamilifu katika maisha na
utume wa Kanisa. Kanisa litumie fursa kama vile michezo na teknolojia mpya za mawasiliano
ya jamii kuwashirikisha na kuwaonjesha vijana kweli za kiimani.
Baba Mtakatifu
anawataka waamini wa Jimbo kuu la Roma kufanya upembuzi yakinifu katika mambo yanayopelekea
watu wengi kujikuta wakiwa wamebaki kama watoto yatima; kugundua tena na kuimarisha
tunu bora za maisha ya kifamilia pamoja na kukazia umuhimu wa Parokia kama Jumuiya
ya Ukarimu. Makleri waendelee kujisadaka katika maisha na utume wao wa Kikuhani kwa
ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Mapadre wawe wapesi kusikiliza
na kutoa huduma kwa wazee, wagonjwa pamoja na kushiriki katika misiba ya wanaparokia
wao. Wajitahidi kuhakikisha kwamba, hakuna mtu anayefariki Parokiani kwao bila kupata
huduma ya maisha ya kiroho pale inapowezekana! Kwa njia hii, Kanisa linaweza kutoka
kifua mbele kwa ajili ya Uinjilishaji. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru waamini
wote waliohudhuria kwa uvumilivu na upendo wao na amewataka kuendelea kumwombea katika
maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.