Kanisa halina budi kuwa huru ili kuonesha ujasiri!
Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa
Jumuiya ya Kanisa Anglikani duniani wakati alipokuwa anazungumza na Baba Mtakatifu
Francisko, Jumatatu tarehe 16 Juni 2014 mjini Vatican amesema kwamba, Kanisa halina
budi kuwa huru na kuonesha ujasiri wa kusimama kidete kulinda na kutetea amani, utu
na heshima ya binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo
ambayo yanaendelea kumdhalilisha binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kuna
maelfu ya watu wanaoendelea kutolea ushuhuda wa maisha yao kwa ajili ya Kristo na
Kanisa lake, hali aliyojionea mwenyewe kwenye kumbu kumbu zinazohifadhiwa kwenye Kanisa
kuu la Mtume Bartolomeo lililoko mjini Roma. Ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki na
Kanisa Anglikana unaweza kusaidia katika mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu
ya binadamu na kwamba, hii ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake,
kumbe wanapaswa kuitumia kikamilifu, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.
Askofu
mkuu Justin Welby amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujasiri na ushuhuda aliouonesha
hivi karibuni kwa kuwaalika Marais wa Palestina na Israeli kusali kwa pamoja ili kuombea
amani na upatanisho huko Mashariki ya Kati. Umoja na ushirikiano miongoni mwa Makanisa
inaweza kuwa ni changamoto katika kulinda, kutetea na kudumisha amani sehemu mbali
mbali za dunia.
Askofu mkuu Welby amempongeza Baba Mtakatifu kwa misaada ya
hali na mali anayoendelea kutoa kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Amerika ya Kusini
pamoja na mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa. Jambo la msingi
ni kuangalia mambo yanayounganisha Makanisa haya mawili kuliko yale ambayo ni kikwazo
na mwendelezo wa utengano.
Novemba mwaka 2014, Kanisa Katoliki litaadhimisha
kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha
Waraka kuhusu Majadiliano ya Kiekumene, Unitatis Redintegratio. Na mwaka 2016 itakuwa
ni kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu tangu Askofu mkuu Ramsey alipomtembelea Papa Paulo
VI na kumzawadia pete yake ya kipapa.
Askofu mkuu Welby anasema, kuna ushirikiano
mkubwa kati ya Kanisa Anglikani na Kanisa katoliki nchini Uingereza, kwani wamekuwa
na fursa mbali mbali za kusali, kuamua na kutenda kwa kushirikiana na Kardinali Vincent
Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza.