Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 15 Juni 2014 ametembelea Jumuiya ya
Mtakatifu Egidio na kukutana pamoja na kusali na maskini, wazee, wakimbizi na wale
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii mjini Roma. Ameishukuru Jumuiya ya Mtakatifu Egidio
kwa kukuza na kudumisha moyo wa sala, kama kielelezo cha ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza
na kuonesha ukarimu kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Neno la Mungu
ni huduma ya kwanza inayotolewa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na hivyo kuwawezesha
kuchota nguvu inayobubujika kutoka katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu,
tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Maskini hata katika umaskini
wao wanaweza kusaidiana na hivyo kuunda Jumuiya inayojipambanua kwa kuwasaidia maskini,
wazee na watoto, kielelezo makini cha Jamii inayojali na kuwajibika.
Wazee
wanapokumbana na upweke hasi wanakata tamaa na hiki ni kielelezo hasi cha Jamii, changamoto
kwa vijana na wazee kuchangamana na kusaidiana kwa kutambua kwamba, sala zao ni zawadi
kubwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Jamii isiyotunza wazee na vijana, haina matumaini
kwa siku za usoni. Sera na mikakati ya uchumi na maendeleo haina budi kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Inasikitisha kuona kwamba, kuna idadi
kubwa ya vijana wasiokuwa na fursa ya ajira na Barani Ulaya, mwaliko wa kulisaidia
Bara hili kurudia tena mizizi ya maisha yake!
Maskini wakiwezeshwa wanaweza
kufanya maajabu katika ustawi na maendeleo ya kijamii, lakini mikakati na uchumi wa
maendeleo katika ulimwengu wa utandawazi unaendelea kuwatenga na kuwatumbukiza maskini
katika baa la umaskini wa hali na kipato, kwa kukosa fursa za ajira na makazi bora
na salama na matokeo yake, kuna umati mkubwa wa watu wanaotengatanga barabarani kutafuta
riziki ya maisha. Mshikamano wa kidugu, ni matusi kwa baadhi ya watu! Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio ni kielelezo cha mshikamano wa upendo na watu wasiokuwa na makazi, wazee na
wakimbizi wanaotafuta maisha bora ugenini.
Baba Mtakatifu anasema wakimbizi
ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita na majanga asilia; ni watu wanaotafuta amani
na usalama wa maisha yao, mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa kweli
ni vyombo vya ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu, kwa kujikita katika sala
na majadiliano zaidi, kwa watu kutambua na kuthamini utambulisho wao pamoja na kuendeleza
majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga umoja na urafiki kati ya watu wa mataifa.
Baba
Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kuwataka wanajumuiya ya Mtakatifu Egidio kujikita
katika maisha ya sala, huduma makini kwa maskini pamoja na kuendelea kuwa ni wajenzi
wa amani na upatanisho sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni chemchemi ya mageuzi ndani
ya jamii.