2014-06-16 11:45:42

Rushwa na ufisadi vinalipwa na maskini!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 16 Juni 2014 anasema kwamba, madhara yanayosababishwa na wala rushwa na mafisadi yanalipwa na maskini na kwamba, dhambi ya rushwa imekuwa sugu tangu kwenye Agano la Kale kama inavyojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu kwa siku ya Jumatatu. Ili kuishinda dhambi hii kuna haja kwa watu kujikita katika huduma makini kwa jirani ili kujenga dhamiri nyofu.

Baba Mtakatifu anatafakari kuhusu shamba la mizabibu la Nabothi aliyeombwa na Mfalme kumwachia shamba hilo ili aweze kupanua bustani yake, lakini Nabothi akakataa kwa kuwa ulikuwa ni urithi wake kutoka kwa mababa zake. Yezebeli mke wa Mfalme akamfanyia hila Nabothi kwa kumpachika mashitaka ya uongo na hatima yake anapigwa mawe hadi kufa. Mfalme akalitaifisha shamba hili kana kwamba, hakuna jambo lolote lililotendeka. Hivi ndivyo wanavyofanya baadhi ya viongozi wenye mamlaka kisiasa, kijamii hata wakati mwingine kiroho. Baba Mtakatifu anasema fisadi na mla rushwa hana dini wala rangi kwani ni watu wanaojisikia kuwa kama miungu wadogo!

Wala rushwa na mafisadi ni watu wanaotaka kujihakikishia usalama wa maisha yao kwa kujitafutia utajiri wa mali na fedha na baadaye madaraka, lakini yote haya ni ubatili mtupu! Maskini na watu wa kawaida ndio wanaolipa madhara yanayofanywa na wala rushwa na mafisadi, kwa kukosa huduma msingi katika sekta ya afya, elimu na maendeleo.

Kwa Makleri wala rushwa na mafisadi, madhara yao yanawatesa waamini wao wanaoshindwa kupata huduma makini za maisha ya kiroho na kimwili. Njia makini ya kuondokana na kishawishi cha rushwa na ufisadi ni kutoa huduma makini kwa jamii, kwa kujijengea moyo wa unyenyekevu ili kushinda kiburi na majivuno, kwani huduma humnyenyekesha mtu!







All the contents on this site are copyrighted ©.