Kardinali Leonardo Sandri, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki
akiungana pamoja na wakuu wa Mashirika na wafanyakazi wa Baraza hili anapenda kuonesha
mshikamano wa dhati na Patriaki Luis Sako wa Kanisa la Wakaldei wa Babilonia, tangu
kuchaguliwa kwake amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, waamini wa Makanisa
mbali mbali wanajikita katika mchakato wa majadiliano na upatanisho wa kitaifa.
Kwa
namna ya pekee, Baraza la Kipapa linapenda kuonesha pia mshikamano wake kwa wananchi
wa Iraq wanaokabiliana na machafuko ya kisiasa ambayo yamepelekea maelfu ya watu kuyakimbia
makazi ili kuyasalimisha maisha yao, kiasi cha kusababisha maafa na usumbufu mkubwa.
Makanisa na Taasisi zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Iraq ziko wazi kwa ajili
ya kutoa hifadhi kwa wakimbizi. Kanisa linashirikiana na viongozi wengine wa dini
kuwasaidia wakimbizi hawa kwa hali na mali.
Ni matumaini ya Baraza la Kipapa
kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kwamba, Sala ya kuombea amani Mashariki ya Kati
wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, itazaa matunda kwa wananchi wanaoishi
Mashariki ya Kati.