Makanisa yanachangamotishwa kuimarisha urafiki, upatanisho na umoja wa Wakristo!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 16 Juni 2014 amekutana na ujumbe wa Askofu
mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa
Anglikani. Baba Mtakatifu amefanya mazungumzo ya faragha kwanza na Askofu mkuu Welby
na baadaye akazungumza na ujumbe wake na hatimaye wakasali kwa pamoja kama njia ya
kuimarisha urafiki na mchakato wa upatanisho na umoja miongoni mwa Wakristo!
Baba
Mtakatifu anasema, mbele ya jicho la huruma linalooneshwa na Yesu, wakristo hawawezi
kuendelea kufumbia macho kashfa ya utengano iliyoko mbele yao kama kikwazo cha utangazaji
wa Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu. Wakristo wanaendelea kubeba mzigo wa utengano
uliojitokeza katika historia ya Kanisa, kiasi kwamba bado wanaelemewa na ubinadamu
kiasi cha kushindwa kutangaza Injili kadiri ya amri ya Kristo.
Umoja wa Wakristo
ndilo lengo la majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo, changamoto iliyotolewa
na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican inayowataka Wakristo kuendelea kushirikiana bila
kuweka kikwazo chochote katika maongozi ya Mungu kwa kuendelea kumtegemea Roho Mtakatifu
anayewakirimia imani na nguvu.
Kama wafuasi wa Kristo wanatambua kwamba, imani
imewafikia kutokana na ushuhuda wa watu wengi. Kumbe, wana deni mbele ya watakatifu,
walimu na Jumuiya ambazo zilijitahidi kutangaza imani katika historia jambo linalowaunganisha
pamoja.
Askofu mkuu Welby, katika maadhimisho ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu,
alisali masifu ya jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Gregori mkuu, mahali ambapo
Agostino na wenzake walipata utume wa kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini
Uingereza na hapo ukawa ni mwanzo wa historia ya imani na utakatifu kwa ajili ya mafao
ya watu wengi Barani Ulaya. Hii ni hija tukufu ambayo imeacha vielelezo vya kudumu
kama vile taasisi na Mapokeo ya Kanisa ambayo ni urithi wa Makanisa msingi wa udugu.
Tume
ya kimataifa ya pamoja kati ya Waanglikani na Wakatoliki na Tume ya Kimataifa ya Umoja
kati ya Waanglikani na Wakatoliki ni muhimu sana katika kutathmini hali ya sasa kwa
kuangalia changamoto zilizopita na zile zilizopo katika dhamana ya kiekumene.
Kwa
mara ya kwanza viongozi hawa wawili walipokutana walizungumzia kuhusu majanga yanayomwandama
mwanadamu katika ulimwengu huu, yaani biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo;
mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko
anampongeza Askofu mkuu Welby kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu na matokeo yake ni ushirikiano wa kiekumene pamoja na Jumuiya ya Kimataifa;
mambo ambayo Kanisa Katoliki na Kanisa Anglikani yanashirikiana sehemu mbali mbali
za dunia. Mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu hususan kwa wanawake kazi
inayofanywa na mashirika mbali mbali ya kitawa ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa.
Baba Mtakatifu anamwalika Askofu mkuu Welby kuendelea kushirikiana kwa pamoja
katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo, kwa kukomesha na kuwasaidia wahanga wa
biashara hii. Kama wafuasi wa Yesu wanatumwa kuganga madonda ya ulimwengu.