2014-06-14 10:59:25

Syria inahitaji misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa!


Viongozi wa wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni hivi karibuni walifanya mkutano chini ya uongozi wa Patriaki Karekin wa Pili, Kiongozi mkuu wa Waamini Wakatoliki wa Armenia, ili kuangalia kwa pamoja changamoto za kiimani zinazoendelea kujitokeza nchini Syria kwa wakati huu.

Kwa pamoja wanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wameomba kuondolewa kwa vikwazo vya kugharimia huduma za kibinadamu zinazotolewa na Mashirika ya Misaada Kimataifa; kusitisha biashara haramu ya silaha inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao pamoja na kuondoa majeshi ya kukodiwa kutoka nje ya Syria yanayoendesha vita nchini humo!

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa upatikanaji wa amani na utulivu nchini Syria baada ya mazungumzo ya awamu ya kwanza na ile ya pili mjini Geneva kushindwa kuzaa matunda yaliyokuwa yanakusudiwa. Wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaoishi katika nchi jirani wapatiwe misaada ya kibinadamu. Ni wajibu wa viongozi na wadau mbali mbali wa Syria kuanza kujitika katika upatanisho wa kitaifa kwa kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limewataka wale waliowateka nyara Maaskofu kutoka Aleppo kuwaachilia maramoja pasi na masharti ili waweze kuungana na ndugu zao katika kutoa huduma za kichungaji.All the contents on this site are copyrighted ©.