Kitendawilitega cha kiswahili, “tatu tatu mpaka pwani,” ni rahisi sana kukitegua kwa
wapishi wa jiko la kienyeji, kwani watayakumbuka mara moja mafiga matatu yanayotegemeza
chungu jikoni. Kumbe kwa asiye mkristo anaposikia juu ya Sikukuu ya Utatu Mtakatifu
anaona hiyo kuwa ni kufuru nzito sana kwa Mungu isiyostahili msamaha.
Aidha
kwetu Wakristo, sikukuu hii inaonekana kuwa ni kitendawilitega kikuu cha imani kisicho
na jibu wala na mteguaji. Tunabaki kusema kuwa hilo ni “Fumbo la Imani”. Aidha kama
Utatu upo, basi sikukuu hii ni ya Utatu Mtakatifu hainihusu mimi na iko mbali sana
nasi na haigusi kabisa maisha yetu.
Ama kweli “Jambo usilolijua litakusumbua”.
Ndugu zangu, Sikukuu ya Utatu siyo kitendawilitega, tena basi ni sikukuu yako kabisa.
Jibu na mteguaji wa kitendawili cha Sikukuu ya leo ni wewe mwenyewe, wala usiepe majukumu.
Hoja ni kwamba, ukifanya tafakari ya maisha yako kwa dhati utagundua mara moja kuwa
sikukuu hii ni yako wewe. Yaani, ni sikukuu inayotokana na mang’amuzi ya maisha yako
na katika ulimwengu wako huu. Utatu ni ukweli halisi unaouishi binadamu lakini kwa
bahati mbaya pengine hatuufanyii tafakari. Mapato yake unabaki kuwa kama uliyelibeba
shoka begani huku unajisumbua kulitafuta ukipita kuliuzia kwa wengine.
Ukipata
kitendawili kama hiki: “Sikukuu ya Utatu ni nini? Wewe jibu kwanza kirahisi tu kuwa
ni Sikukuu ya “Muungano” au “Jamhuri ya Muungano”. Jamhuri ni neno la kiarabu lenye
maana ya watu, au taifa na kwa kiingereza ni public, au – republic linalotokana na
maneno mawili ya la kilatini – res (vitu, mali, raslimali, tunu) na – publicum (watu,
umma, taifa). Kwa hiyo Jamhuri – republic, ni kuunganisha raslimali ya watu na taifa
au maamuzi ya watu au ya taifa kuwa ya umma. Katika uwanja wa siasa Jamhuri ya Muungano
– United Republic humaanisha muunganiko wa mataifa mawili au zaidi na raslimali zao
za umma na kufanya kuwa Taifa moja.
Kwetu sisi, Sikukuu ya leo ya Fumbo la
Utatu Mtakatifu ni ufunuo au ufumbuzi wa siri ya maisha, ni chemchemi ya hekima ya
maisha ambayo msingi wake ni kuelewa uhusiano, umoja wa mambo, wa hali, wa nafsi nk.
Kwa hiyo tungeweza kusema kuwa leo ni sikukuu ya “Muungano.” Kimsingi na kwa uasili
wake, kipeo cha muungano wowote ule kinatokana na muungano wa kifumbo ulio katika
Mungu.
Lakini awali ya yote budi ieleweke kuwa Mungu ni mmoja tu, hakuna Mungu
wawili au watatu au zaidi. Halafu, yabidi uelewe na utoe maelezo kwamba Mungu huyu
kwa yeye mwenyewe siyo jiwe lisilo na uhai, bali anazo sifa nyingi sana zilizoungana
katika yeye, yaani Mungu ni tajiri sana na mwingi wa raslimali zilizoungana katika
yeye na mwenye makakala – nguvu (dynamic).
Kwa hiyo, Mungu siyo “upweke” bali
ni “muungano”. Aidha, makakala (dynamism) hayo katika Mungu yanaunganishwa na upendo
ulio wa milele katika yeye. Kwa hiyo ukitaka kumwelewa Mungu na utajiri wake unaounganishwa
na upendo, usitumie njia ya kiakili au njia ya kiutaalamu au ya kidhahania (kimawazo),
bali tumia njia ya mang’amuzi ya maisha ya kawaida kabisa, yaani wewe umtazame binadamu,
umfanyie fikara na umtafakari kidhati binadamu jinsi alivyo “muungano” wa mambo makuu
katika yeye.
Kwa hiyo “fumbo umfumbie mjinga” kwa sababu jibu la fumbo hili
unalipata kwa wewe binadamu mwenyewe. Tukifajitafakri kidogo tu, tutagundua kirahisi
kwamba, binadamu kwanza anayo maisha, uzima au uhai ambao tunajua tumeupata toka kwa
Mungu aliyetuumba; pili, katika maisha hayo, tutagundua kuwa binadamu tunahitaji upendo,
yaani kujipenda, kupenda na kupendwa na wengine ili tuweze kuendeleza maisha. Tatu,
tutagundua pia kwamba, katika binadamu kuna hatima ya maisha tuliyopangiwa na Mungu,
yaani mwisho wa maisha yetu ambayo siyo kifo tu, bali tutaendelea kuishi na Mungu
aliyetuumba.
Ili tuweze kuelewa kiundani muungano wa hali hizi tatu, tunaweza
kusema kwamba utatu ni hekima au busara ya kujua ni kitu gani hayo maisha, uhai na
uzima; halafu ni busara ya kujua ni nini huo upendo; na mwisho ni busara ya kutambua
ni nini hatima au mwisho wa binadamu. Kwa hiyo, endapo Utatu ni hekima ya maisha,
ya upendo na ya kifo, basi Utatu huu unafaa kuutathmini kwa sababu unaeleza hali halisi
ya uwepo wa binadamu. Hebu sasa tuuangalie muungano huo katika binadamu kisha tuulinganishe
na Sikukuu ya muungano wa Utatu Mtakatifu tunayosherekea leo, tukiongozwa na Injili
ya leo.
Utatu ni Uzima, au Uhai wenye asili yake kwa Mungu: Hapo mwanzo
Mungu alipotaka kumwumba binadamu alisema: “Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura
yetu” (Mwanzo 1:26). Mungu ametupa uhai, maisha na uzima (ametuumba) na tunafanana
naye. Kwa hiyo, Mungu ni utajiri wa uhai na uzima alio nao hadi akasema: “tufanye”,
na utajiri huo wa uzima ametushirikisha sisi kwa kutuumba.
Aidha kufanana kwetu
naye siyo na Mungu mwumbaji au na Roho au na Neno la milele, bali ni utajiri wa uhalisia
huo wote wa Mungu kijumla. Ni muungano au uhusiano ambao ni msingi wa ndani kabisa
wa Mungu na binadamu. Mtu ameumbwa kwa mfano wa mahusiano na wa muunganiko huo. Kwa
sababu upweke ni kinyume na hali aliyoumbwa nayo binadamu upweke huo unatisha na hauvumiliki.
Ndiyo maana ninapokaa pamoja na wengine ninajisikia vizuri, kwani huo ndiyo wito wangu.
Kwa hiyo kama Mungu wetu asingekuwa na utajiri uhai ulioungana hadi akajitoa
zawadi, tusingeshirikishwa uhai wake na tusingeweza kufanana naye na hivi huyo asingekuwa
Mungu, badala yake angekuwa Mungu wa kufikirika na wa kidhahania tu. Kumbe huyo siyo
Mungu wa kimawazo, bali daima anajitoa, daima anatukirimu, daima anatoka na kutujia
ili kuwa nasi. Mungu huyo yupo daima katika harakati.
Utatu ni Upendo wenye
asili yake kwa Mungu Bila upendo hakuna muungano na ushirikiano na wala hakuna
umoja. Kwa hiyo utatu ni muungano wa upendo, ambao Injili inatangaza wazi leo: “Kwa
maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee” (Yoh. 3:16).
Aya hiyo ndiyo kiini cha Injili ya Yohane anayesema: “Mungu ni upendo” (IYoh 4:8-16)
na anatutaka sote tukiri na kusema kwa kustaajabia: “Nasi tumelifahamu pendo alilo
nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini.
Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo,
hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” (IYoh. 3:16). Kwa hiyo watu wanapokuuliza
wewe mkristu: “unasadiki nini?” Jibu tunalotegemea daima ni lile la kutoka kitabu
cha katekisimu ya kanisa: “Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi muumba mbingu na dunia;
na kwa Yesu Kristu Mwanae wa pekee, aliyesulibiwa na kufufuka. Nasadiki kwa kanisa
moja takatifu….” nk.
Ni sawa kabisa jibu hilo. Lakini swali hilo hilo ukimwuliza
yeyote asiye mkristu “Wewe unasadiki nini hapa duniani?” Utapata majibu mengi sana
na mwingine atakuambia “mimi sisadiki Mungu” wakati hujamwuliza swali la Mungu. Lakini
jibu moja linaloweza kutolewa na wote bila kujali itikadi zao za dini au uraia, utamaduni
wala elimu, ni kwamba binadamu yeyote yule anasadiki juu ya Upendo. Hilo ndilo jambo
muhimu, kwa sababu kila mtu, kila kiumbe, hata asiyesadiki chochote au asiye mwamini
anaweza kulisadiki pendo, anaweza kujiaminisha au kusadiki juu ya upendo kama ndiyo
busara pekee ya maisha.
Asiyesadiki juu ya upendo huyo yuko katika laana ya
maisha yasiyo na uzuri wowote. Ndivyo hivyo anavyotuambia Yohane “Sisi tumesadiki
juu ya upendo.” Ukisadiki katika utajiri ulio katika upendo, hapo unakumbana na Jamhuri
nyingine ya muungano, kwani tendo la kupenda daima linaenda pamoja na tendo jingine
zito nalo ni kutoa.
Kwa hiyo, kupenda ni sawa na kutoa au kujitoa. Huwezi
kutoa usichokuwa nacho – nemo dat quod non habet. Kama unatoa maana yake una kitu
cha kugawa. Mungu anapenda kwa vile anatoa, hivi Mungu amefurika upendo. Mwinjili
anatuambia: “Mungu aliupenda sana ulimwengu hata akamtoa Mwanae wa pekee.” Utajiri
mkuu wa Mungu ndiyo Upendo ambao ni Yesu Kristu aliye Mungu. Yohane anasema tena “Mungu
aliupenda mno ulimwengu.” Hakumpenda binadamu peke yake bali aliupenda pia ulimwengu,
dunia, wanyama, mimea na uumbaji wote kijumla. Mungu ametoa uhai kwa wote bila ubaguzi.
Endapo yeye ameupenda ulimwengu, nami pia yanibidi kuipenda dunia hii, watoto wake,
mimea, maua, nk. Kwa hiyo, katika upendo tusijiulize tunaweza kupokea nini toka kwa
wengine, bali tujiulize sisi tunaweza kutoa nini kwa wengine.
Utatu ni Hatima
yenye mwanzo na mwisho (Alfa na Omega) kwa Mungu siyo hukumu. “Mungu hakumtuma
Mwanae ulimwenguni ili kuuhukumu, bali kusudi ulimwengu uokolewe.” Maana ya kuokoa
ni kuwa na fikra potovu na ya kutisha ya “Kufabasi”. Kifo siyo hatima yetu, bali hatima
yetu ni kukaa na Mungu. Mungu anapenda kuokoa, kutoa maisha, kutufanya sisi sote kuwa
watoto wake. Mungu anatoa maisha yake, anataka kutukomboa sote tuwe waana katika Mwana,
na tuendelee kuishi naye milele. Yohane anatutaka tusafishe fikra mbovu tulizo nazo
juu ya Mungu, anataka kutuondolea woga juu ya Mungu yaani tutoe picha ya Mungu aliye
mkali na anayeadhibu na kwamba kifo siyo hatima yetu ya mwisho.
Kwa hiyo, sikukuu
ya utatu ni kioo cha undani wa moyo wangu kinachonionesha nimetoka wapi, niko wapi
na hatima yangu na ya ulimwengu huu ni ipi. Siku ya leo ni sawa na kusherekea kwa
pamoja sikukuu tatu za maisha yangu, yaani kuzaliwa (uzima, uhai, maisha), ndoa (mwito
wowote – upendo) na kifo (hatima, umilele). Kwa hiyo Utatu ni Mungu aliye Uzima wote,
Upendo wote na asiye na hatima, Anadumu milele yote. Sisi pia tunatembea katika Muungano
huo na tupo safarini kuelekea umilele (hatima) usiyo na mwisho, kwenye Jamhuri ya
Muungano Mtakatifu. Kumbe leo ni Sherehe ya Jamhuri ya Muungano wa undani wangu, maisha
yangu, upendo wangu na hatima yangu. Asili ya muungano huo ni utajiri mkuu wa muungano
ulio katika Utatu Mtakatifu wa Mungu Mmoja. Heri kwa Sikukuu ya Utatu Mtakatifu.