2014-06-14 11:47:53

Papa Francisko anawachangamotisha watu kujikita katika ukweli, uwazi na uaminifu!


Kiongozi wa kidini Dalai Lama anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa mafundisho yake makini, utashi, ukweli na uwazi. Ni kiongozi anayeonekana kuonesha ujasiri katika utekelezaji wa dhamana na utume wake, kwa kuwahamasisha watu kuona, kutambua na kumwilisha katika uhalisia wa maisha yao tunu ya: ukweli, uwazi na uaminifu, mambo ambayo kwa sasa yanaonekana kukosekana kwa miongoni mwa watu wengi.

Dalai Lama ameyasema hayo katika mahojiano maalum na Gazeti la "Corierre dela Sera" linalochapishwa nchini Italia. Anasema, Wakatoliki na Wabudha wanayo mambo mengi yanayowaunganisha pamoja, kwani dini kuu duniani zinataka kutangaza ujumbe wa amani na mapendo. Jambo linaloweza kuchafua na hatimaye kufanya amani itoweke katika jamii ni chuki, hasira na uhasama unaojengeka kati ya watu.

Dhamana na wajibu wa dini katika mazingira kama haya ni kusaidia mchakato wa kuponya madonda na hivyo kuanza toba, wongofu na upatanisho wa kweli. Watu wajifunze kuheshimiana na kusameheana kwani kukosa na kukosehana ni sehemu ya ubinadamu.

Dalai Lama anasema, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amewakumbusha walimwengu kwamba, imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda ni sawa na chanda na pete; ni mambo yanayokwenda pamoja na kamwe hayawezi kutenganishwa. Imani bila uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda, iko mashakani na daima itayumba! Sayansi inajikita katika uwezo wa mwanadamu kufikiri. Anasema kwamba, ana wasi wasi mkubwa ikiwa kama sayansi peke yake bila kumwilishwa katika imani inaweza kumletea mwanadamu maendeleo ya kweli.

Uvumbuzi wa nyuklia ni mafanikio makubwa katika ulimwengu wa sayansi na maendeleo ya mwanadamu, lakini bila kuongozwa na kanuni maadili, mafanikio yote haya yanamjengea mwanadamu hofu na mashaka katika mchakato wa ustawi na maendeleo yake kwa sasa na kwa siku za usoni!







All the contents on this site are copyrighted ©.