Jumuiya ya Kimataifa imeamua kuwavalia njuga wanajeshi wa Kikundi cha Kigaidi cha
Boko Haram kinachoendelea kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wasiokuwa na hatia
ndani na nje ya Nigeria. Mawaziri wa mambo ya Nchi za Nje kutoka Uingereza, Benin,
Cameroon, Ciad, Niger, Umoja wa Ulaya, Canada na Marekani, Ijumaa tarehe 13 Juni 2014
wamekutana na kujadili tatizo hili na changamoto zake katika kulinda na kudumisha
amani na usalama nchini Nigeria na katika nchi jirani ambao pia wanatishiwa na mashambulizi
ya kigaidi kutoka kwa Kikundi cha Boko Haram.
Mawaziri hawa walikuwa wanashiriki
katika mkutano wa kimataifa uliokuwa unatafuta mbinu za kupambana na hatimaye kusitisha
kabisa nyanyaso za kijinsia katika maeneo ambamo vita inaendelea kurindima. Jumuiya
ya Kimataifa inaendelea kuonesha mshikamano wa hali na mali katika harakati za kutaka
kuokoa maisha ya wasichana waliotekwa nyara na Boko Haram, Kaskazini mwa Nigeria.
Uingereza
itaongeza msaada wake wa kijeshi na huduma katika sekta ya elimu nchini Nigeria, ili
amani na utulivu viweze kurejea tena!