Gawio la Tanzania kutoka TIPER kuelekezwa katika sekta ya elimu, afya na maji
Serikali ya Tanzania imepokea shilingi bilioni moja kutoka TIPER ikiwa ni gawio ambalo
kampuni hiyo imekuwa ikilipa kwa Wanahisa wake kila mwaka. Kauli hiyo imetolewa na
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servarcius Likwelile alipokuwa akipokea gawio hilo
katika hafla iliyofanyika Ijumaa tarehe 13 Juni 2014 mjini Dodoma.
Dkt.
Likwelile alisema kuwa gawio hilo litaelekezwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha
2013/2014 unaomalizika kwa kuangalia maeneo ambayo yanawagusa wananchi ikiwemo sekta
ya elimu, afya na maji. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Daniel
Belair alisema kuwa si mara ya kwanza kwa kampuni yake kutoa gawio kama hilo kwa Serikali
ambapo mwaka jana muda kama huu kampuni ilitoa kiasi kama hicho kama gawio.
Mkurugenzi
huyo alisema kuwa kampuni yake imeendelea kufanya vizuri katika kukuza maisha ya kijamii
na kiuchumi ambapo kwa sasa inafanyakazi kwa saa 24 na siku saba za wiki. Kwa kuzingatia
utendaji huo, kampuni ya TIPER imekuwa kichocheo kukuu cha kuzalisha ajira nchini
ambapo hadi sasa asilimia 99 ya wafanyakazi wake ni nguvu kazi ya Watanzania.
Naye
Mwenyekiti Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi ya TIPER Prof. Abdulkarim Mruma alisema
kuwa imekuwa ni muhimu kwa kampuni yao kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta kwa nchi
na kuleta mafanikio makubwa ya upatikanaji wa mafuta nchini. Aidha, TIPER Prof. Mruma
alisema kuwa kwa sasa kampuni yao imejikita katika kuleta mafuta yaliyosafishwa nchini
ili kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.
“Kwa sasa tunaleta mafuta yaliyosafishwa
badala ya mafuta ghafi ambayo yanazalisha tope jingi ambalo limekuwa ni hatari katika
kutunza mazingira yetu” alisema Prof. Mruma. Pamoja na ufanisi huo, kumekuwepo na
changamoto za kuboresha mkataba wa utendaji na usimamizi wa hesabu masuala ambayo
wanahisa wote wawili wanaendelea kuyafanyia kazi kwa madhumuni ya kuwa na matokeo
mazuri zaidi kwa pande zote.
Kiutendaji kampuni ya TIPER inaendeshwa kwa
ubia kati ya Serikali ya Tanzania ambayo ina hisa zenye asilimia 50 na Kampuni ya
Oryx Energies SA asilimia 50. Pamoja na Tanzania Kampuni ya Oryx Energies SA inafanyakazi
katika nchi mbalimbali duniani ambazo ni Benin, Burkina Faso, Côte d'Ivoire, Guinea
Conakry, Kenya, Mali, Niger, Nigeria, Senegal, Sierra Leone, Afrika Kusini, Hispania
(Visiwa vya Canary), Togo, Uganda na Zambia.