2014-06-14 12:19:13

Familia ni kiini cha yote!


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani katika mkutano wake wa mwaka uliofunguliwa hapo tarehe 11 hadi tarehe 13 Juni 2014 huko New Orleans umejadili pamoja na mambo mengine umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Mada hii inakwenda sanjari na maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu Katoliki kuhusu familia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba mjini Vatican. Haya pia ni maandalizi ya Siku ya Familia Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia hapo Septemba 2015 na Baba Mtakatifu Francisko amealikwa kuhudhuria tukio hili linaloonesha vipaumbele vya kichungaji kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa nyakati hizi.

Matukio yote mawili ni fursa muhimu sana kwa Kanisa kupembua kuhusu: tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; dhamana na utume wa familia katika maisha ya Kanisa na mchango wa familia katika kuimarisha mahusiano ya kijamii.

Akichangia mada kuhusu familia kwenye mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anabainisha kwamba, lengo la maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani ni kuonesha upendo ambao mwanadamu anapaswa kuoneshwa na kushirikishwa. Injili ya Familia haina budi kuvuka mipaka ya ubinafsi na upweke katika maisha ya watu.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema ndani na nje ya Marekani wanahamasishwa na Mama Kanisa kushiriki katika matukio yote haya mawili kwa uwepo wao mkalimifu au kwa njia ya sala. Maadhimisho haya kwa Marekani itakuwa ni fursa ya kutangaza Injili ya Furaha pamoja na kupyaisha maisha ya ndoa na familia. Waamini watapata fursa ya kutafakari asili ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu; mafundisho tanzu kuhusu ndoa na familia kadiri ya Kanisa Katoliki.

Askofu mkuu Paglia anasema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya imani na kumong'onyoka kwa tunu msingi za maadili na utu wema; kwani hapa mtu binafsi na haki zake binafsi anapewa kipaumbele cha kwanza kuliko tunu msingi na haki za familia. Kuna baadhi ya nchi zinatunga sheria kwa kuzingatia mahitaji ya mtu binafsi na kuzitenga familia katika mchakato huu.

Kutokana na mantiki hii inaonekana kwamba, familia sehemu mbali mbali za dunia zinaendelea kubezwa kana kwamba hazina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya watu. Kuna sehemu ambako familia zinaendelea kunyanysika na kudhulumiwa kisheria! Zote hizi ni changamoto katika maisha ya ndoa na familia! Mazingira yote haya yanapelekea watu kupendelea zaidi upweke kuliko kufanya maamuzi ya kuanzisha familia.

Lakini familia inayojadiliwa na kupigiwa debe na Mama Kanisa ni kadiri ya mpango na utashi wa Mungu kwa binadamu na wala si vinginevyo! Familia itaendelea kuwa ni rasilimali kubwa katika ustawi na maendeleo ya Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.