2014-06-13 07:26:48

Silaha za kinyuklia zinatishia amani na usalama duniani!


Askofu mkuu Francis Chullikatt, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni alipokuwa anachangia mada kuhusu mkataba wa umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa silaha za kinyuklia alisema kwamba, umefika wakati kwa nchi zinazozalisha silaha za kinyuklia kusitisha biashara hii ambayo kamwe haikubaliki kimaadili. RealAudioMP3

Hii ni changamoto iliyotolewa na Jumuiya ya Kimataifa miaka 44 iliyopita sanjari na kumbu kumbu ya miaka 25 tangu kusitishwa kwa vita baridi duniani, lakini hadi leo hii bado kuna silaha za kinyuklia zipatazo 17, 000 zilizoenea sehemu mbali mbali duniani, silaha zinazotishia usalama wa maisha na amani ulimwenguni.

Nchi zinazotengeneza silaha za kinyuklia zinaendelea kutumia wastani wad olla za kimarekani billion 100 kwa mwaka kwa ajili ya kuzalisha silaha za kinyuklia. Ikumbukwe kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inahitaji kwa udi na uvumba rasimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia.

Askofu mkuu Chullikatt anabainisha kwamba, kwa miaka mingi, Vatican inaunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupiga rufuku uzalishaji na usambazaji wa silaha za kinyuklia, ili kuondoa wasi wasi na hofu ya mashambulizi na hatimaye mauaji ya alaiki ya watu. Lengo la kuendelea kutoa mwaliko huu ni kutaka kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo endelevu katika kutunza dunia na familia ya binadamu katika ujumla wake.

Hapa anasema Askofu mkuu Chullikatt kuna haja ya kuwa na ushirikiano wa dhati kati ya Nchi zinazotengeneza na kusambaza silaha za kinyuklia na nchi zile ambazo hazina uhusiano wa karibu na silaha za kinyuklia, ili kwa pamoja kuunda chombo cha kisheria kitakachokuwa na nguvu ya kusimamia utekelezaji wa mkataba wa udhibiti wa uzalishaji na matumizi ya silaha za kinyuklia hali ambayo inatishia usalama wa watu wengu duniani, kama ilivyokubalika kunako mwaka 2010.

Bila utekelezaji wa mkataba huu, amani na usalama viko mashakani na kwamba, mkataba wa udhibiti wa silaha za kinyuklia duniani hautakuwa na nguvu tena. Askofu mkuu Francis Chullikatt anasema, mchakato wa udhibiti wa silaha za kinyuklia si vita ambayo imekosa makali, bali ni mwendelezo kwa Jumuiya ya Kimataifa kutambua madhara yake kwani familia ya binadamu ni moja na inategemeana kwa mambo mengi.

Uwepo wa silaha za kinyuklia unatishia amani na usalama, kumbe ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sauti ya mwisho katika udhibiti wa silaha za kinyuklia ili kuweza kuwa na uhakika wa amani kwa kiwango cha kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.