2014-06-13 11:00:50

Lindeni watoto!


Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 12 Juni, inaadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya kazi za suluba kwa watoto wadogo! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano tarehe 11 Juni 2014 alilizungumzia tatizo hili ambalo linaendelea kuwadhulumu, kuwanyonya na kuwanyanyasa watoto kwa kuwafanyisha kazi katika mazingira magumu na hatarishi; kiasi kwamba, wengi wao wanageuzwa kuwa ni watumwa na hata wakati mwingine kubaguliwa!

Baba Mtakatifu Francisko anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwanusuru watoto kutoka katika janga hili la maisha. Kila mtu ndani ya jamii, lakini zaidi, familia ziendelee kuwajibika barabara, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya kila mtoto, ili aweze kupata malezi na makuzi bora. Utoto mtulivu unawahakikishia watoto maisha bora zaidi kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema waliokuwepo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Jumatano asubuhi kusali kwa ajili ya kuwaombea watoto wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu na heshima yao!

Shirika la Kazi Duniani (ILO) linakadiria kwamba, kuna zaidi ya watoto millioni 168 wanaofanyishwa kazi za suluba sehemu mbali mbali za dunia. Umoja wa Mataifa unataka kufuta janga hili kwenye uso wa dunia ifikapo mwaka 2016. Kazi za suluba ni chanzo kikuu cha kudumaa kwa watoto wadogo, kiasi kwamba afya zao zinaathirika vibaya kwa kunyimwa usalama na makuzi stahiki. Asilimia kubwa ya watoto wanaofanyishwa kazi za suluba wako Barani Asia.

Kusini mwa Jangwa la Sahara, watoto zaidi ya millioni 59, wengi wao wakiwa wanatoka Burundi wanafanyishwa kazi za suluba hasa majumbani. Maadhimisho ya Siku hii kimataifa ni kutaka kuibua sera na mikakati itakayosaidia kudhibiti tabia ya kuwafanyisha kazi za suluba watoto wadogo, changamoto kwa familia kutekeleza wajibu na dhamana yao bila kusita. Serikali zikiwa na sera makini zinaweza kusaidia familia zenye kipato cha chini kumudu gharama za maisha; kwa kupata huduma msingi za elimu na afya.







All the contents on this site are copyrighted ©.