Mpendwa msilikilzaji wa Neno la Mungu, leo tunaadhimisha fumbo la Utatu Mtakatifu.
Ni sherehe kati ya sherehe za Bwana ambayo huadhimishwa Dominika inayofuata mara baada
ya Pentekoste.
Mama Kanisa
ameweka sherehe hii baada ya Pentekoste kwa sababu anajua tayari fumbo zima la Utatu
Mtakatifu limekwishafunuliwa kwetu. Na kwa namna hiyo Mama Kanisa apenda kutuingiza
katika furaha ijayo kwetu kila siku kwa njia ya Utatu Mtakatifu. Anatushirikisha fumbo
la Mungu kukaa nasi daima mpaka mwisho wa maisha ya utume wetu hapa duniani. Kwa njia
ya fumbo hili upendo wa Mungu kwa wanadamu unafunuliwa hatua kwa hatua tokea Agano
la kale hadi Agano Jipya.
Mpendwa msiklizaji, kwa hakika kila Dominika
tunaadhimisha sikukuu ya Utatu Mtakatifu. Hata hivyo rasmi kama sherehe kati ya sherehe
za Bwana, sherehe ya Utatu Mtakatifu iliwekwa katika Kalenda ya Liturujia mnamo karne
XIV ili kuadhimisha na kutafakari juu ya asili ya Mungu tunayemwamini. Tunazungumza
juu ya Mungu tunayemwamini, tunataka kupambanua kinaganaga tofauti na uelewa mwingine
juu ya Mungu.
Mfano dhahiri ni kwamba zipo imani nyingine ambazo huamini
kwamba Mungu ni muumbaji wa mbingu na nchi lakini hakushuka kuja duniani, kwa namna
hiyo wanakataa asili ya utu wa Kristu. Wengine watasimama mara tu wanapofika kwa mababu.
Ndiyo kusema masomo yaliyochaguliwa katika sherehe hii yanataka kuweka wazi asili
ya Mungu wetu na kuondoa hisia, picha potofu na uelewa kinyume juu ya asili ya Mungu.
Kwa hakika Mungu wa Kikristu si Mungu peke bali ni familia, ni UTATU.
Mmoja
anaweza kukata tamaa akisikia habari ya fumbo hili kwa maana ya kuwa UMOJA usiogawanyika
na wakati fulani kuonekana katika WINGI=Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mpendwa kimahesabu
mantiki haitupi jibu, kumbe yatupasa kwenda katika mantiki ya Kiteolojia na Kiimani
zaidi. Ndiyo kusema yatupasa kukumbuka kabisa kuwa imani si kukubali kiurahisi habari
ya ukweli wa kidini bali kuukumbatia na kuuishi ukweli huo katika ugumu wake.
Mantiki
hii ndiyo mantiki ya neno kuaamini kwa kiebrania. Kwa njia ya imani lazima kuweka
akili zetu na maonjo yetu kwa Mwenyezi Mungu. Aidha kwa mantiki hiyo, kuwa na imani
si kusadiki katika Utatu Mtakatifu tu bali kuambatana na Utatu Mtakatifu, kuishi katika
Utatu na kujisalimisha na kujitumainisha katika fumbo hilo.
Katika somo
Ia kwanza Mungu anajitokeza na kutangaza asili yake na hivi anarekebisha uelewa wa
watu wa zamani kabla ya ufunuo huo. Watu walielewa kuwa Mungu ni mwenye nguvu, mtawala
anayetisha na mwenye kuadhibu anapokosewa hasa kwa njia ya magonjwa na mikasa mbalimbali.
Kumbe anatangaza asili yake kwa Musa akisema “mimi ni mwingi wa huruma, ni mwenye
fadhila na si mwepesi wa hasira. Picha ya Mungu katika somo hili ni Baba, mwenye mapendo,
anayeelewa shida na makosa ya watoto wake na mara moja kuwasamehe hata wanapotenda
dhambi.
Katika somo la Pili toka barua ya Pili ya Mtakatifu Paulo kwa
Wakorinto, ambayo ni sehemu ya mwisho ya barua hiyo, Paulo anakazia maisha ya mapendo
na kuheshimiana katika jumuiya. Anataja furaha, iliyo ishara ya ujio wa ufalme wa
Mungu katika moyo wa mtu. Ili kuiendeleza furaha hiyo kwa ajili ya wengine anawaalika
kuungana daima katika jumuiya, wakijenga amani na maelewano. Kwa furaha na mshikamano
watakuwa wanaonesha sura ya Mungu katika maisha yao na kwa wengine wasioamini. Baada
ya kuweka vipaji pamoja kwa ajili ya kujenga jumuiya, Mtakatifu Paulo ataweka mbele
yao salaam ambayo daima huitumia kuwasalimu wanajumuiya na pengine Wakorinto walikuwa
wakiitumia katika kupeana amani, yaani ile salaam inayotangaza Utatu Mtakatifu.
Kwa
salaam hii Paulo ataka kuwaambia Wakorinto kuwa, ni Baba anayeanzisha safari ya kuja
kwao yaani kwa ajili ya wokovu wao. Ni Baba ambaye anatunza nafasi yao huko mbinguni
wa ajili ya uzima wa milele. Kisha Baba, Mt Paulo atamtaja Mwana kama yule ambaye
alikamilisha nia ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu. Ni Mwana ambaye kwa njia
ya utii na uaminifu wokovu unamfikia mwanadamu. Aidha Mtakatifu Paulo atamalizia salaam
yake kwa kutangaza uwepo wa Roho Mtakatifu. Kwake yeye Roho ndiye upendo kati ya Baba
na Mwana, ni yule ambaye tumepewa kwa njia ya ubatizo, na twakumbuka wote kuwa wakati
tukipokea zawadi ya Roho Mtakatifu kwa njia ya ubatizo tunakuwa watoto wa Utatu Mtakatifu,
Mungu mmoja.
Kumbe, Mtakatifu Paulo anaposema “neema ya Bwana wetu Yesu
Kristu na pendo la Mungu na ushirika wa Roho Mtaatifu ukae nanyi nyote, atangaza kuwa
sote tunazaliwa toka Mungu mmoja. Wengine hupendekeza kama vile hii ingekuwa ndio
salaam wakati wa kupeana amani, maana yaonesha umoja na mshikamano asilia wa maisha
yetu ya Kikristo.
Katika Injili toka Mwinjili Yohane, tunamwona Bwana akizungumza
na Nikodemo na kiini cha mazungumzo ni upendo upeo wa Mwenyezi Mungu unaojidhihirisha
kwa njia ya kumtoa Mwanae wa pekee. Ni katika mazungumzo haya tunazidi kugundua asili
ya Mungu, kinyume na fikra walizonazo baadhi ya watu, wakifikiri kwamba Mungu ni mpelelezi,
mwenye kuadhibu na kuangamiza, kama si sasa basi anasubiri mwisho wa dunia! badala
yake Mungu ni upendo usiopimika unaobubujika kila siku kwa ajili ya mwanadamu. Hili
tunaligundua toka Injili ya Yohane.
Mpendwa msikilizaji, Yohane akinukuu
maneno ya Bwana anasema kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa
Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminie asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maneno
haya yanaonesha kuwa Mungu si tu mwenye huruma bali ni yule anayependa, kiasi kwamba
anakuja kuishi kati yetu, anajimwilisha kwa ajili ya wokovu wetu! Tena huyu aliyekuja
kwetu si tu alipomaliza miaka yake 33 aliondoka kwa ujumla bali anaendelea kukaa nasi
katika Ekaristi Takatifu na katika sakramenti nyingine. Upendo huu upeo twaweza kujaribu
kuuelewa tukirudi nyuma na kutafakari tendo la Abrahamu kutaka kumtoa sadaka mwanae
wa pekee Isaka, akitufundisha uaminifu na imani kwa Mungu.
Bwana akisonga
mbele katika fundisho lake wa Nikodemo anasema Mungu alipomtuma Mwana haikuwa ili
Mwana auhukumu ulimwengu bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Kumbe Mwana ni kwa ajili
ya kuokoa na si kuangamiza, ni kwa ajili ya kutunza na si kupatiliza mwanadamu. Bwana
ametufundisha kumwita Mungu Baba “Abba” hii inawezekana kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
Mwana ametufundisha na kutuonesha Baba ambaye hajui kulaani bali anajua
kupenda tu. Bwana anasonga mbele akisema yule ambaye haamini basi anajihukumu yeye
mwenyewe kwa sababu hakuliamini jina la Mwana wa pekee wa Mungu. Aya hii kama sehemu
ua Injili ya Yohane inataka kujenga na kuweka wajibu wa mkristu au awaye yote mbele
ya neema zinazofunuliwa kwake. Katika uhuru wake ni lazima aamue kuukumbatia upendo
au kuukataa na hivi hukumu iko katika kukataa kwenyewe. Ndiyo kusema hukumu haisubiriwi
siku ya mwisho bali hujifungamanisha katika kupokea au kutopokea upendo wa Mungu katika
uhuru na utashi kamili wa mtu mwenyewe.
Mpendwa mwana wa Mungu, katika
utangulizi nilijaribu kujenga mantiki ya Utatu Mtakatifu sasa tunaliweka fumbo katika
uhalisia wa maisha ya Kanisa. Kwa kawaida ni fumbo kuu kati ya mafumbo makuu matatu,
yaani fumbo la Ekaristi Takatifu na umwilisho, fumbo la neema za Mungu na Utatu Mtakatifu
ambao ndio tunasherehekea leo.
Ni fumbo ambalo si rahisi kulielewa kwa
undani na ukamilifu wake kwa maana ndiyo Mungu mwenyewe. Tunachotambua ni kuwa, Mungu
Baba ni muumbaji, na alipokwisha kuumba mbingu na nchi alimtuma Mwanae ili aokoe mwanadamu
aliyepoteza uzuri aliokabidhiwa na Mungu Baba na hivi Mungu Mwana ni Mkombozi.
Mwana
alipokwisha kufundisha na kumaliza kazi yake kabla ya kupaa mbinguni alihaidi kumpeleka
Roho Mtakatifu mfariji na mwalimu atakayetukumbusha yote na tena hatafanya kinyume
na yale yaliyofundishwa na Bwana. Kumbe mpendwa msikilizaji Utatu Mtakatifu ni Mungu
mmoja lakini nafsi tatu zisizogawanyika, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kutambua
na kujaribu kuelewa tunahitaji kuwa na imani thabiti kama nilivyokwishadokeza mwanzoni.
Ninakutakieni
sherehe njema, ukajazwe imani, maisha yako yote katika Utatu Mtakatifu. Tumsifu Yesu
Kristu. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.