2014-06-12 08:09:26

Lengo ni kuokoa maisha ya mwanadamu!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kuwa mstari wa mbele katika uhamasishaji wa kuridhia mkataba wa udhibiti wa biashara ya silaha duniani ili kuokoa maisha ya watu sehemu mbali mbali duniani. RealAudioMP3

Kuna maelfu ya watu wanaofariki dunia kutokana na vita huko Syria na Sudan ya Kusini kutokana na biashara haramu ya silaha inayowaingizia wahusika mamillioni ya dolla za kimarekani kwa mwaka, lakini kwao utu, heshima na maisha ya mwanadamu hayana nafasi bali “pochi” imepewa kipaumbele cha kwanza.

Baraza la Makanisa linaendelea kuzihamasisha Serikali mbali mbali duniani ili kuridhia mkataba wa kimataifa utakaodhibiti biashara ya silaha duniani, jambo ambalo si rahisi sana wanasema wachunguzi wa mambo kwani hapa masuala ya uchumi yanapewa kipaumbele cha kwanza kuliko hata uhai wa binadamu.

Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kutoka Barani Afrika wamekuwa wakitaka mkataba wa udhibiti wa silaha kushughulikia pia silaha ndogo ndogo na risasi zinazosababisha maafa au majeraha makubwa kwa watu. Baraza la Umoja wa Mataifa katika mkutano wake wa hivi karibuni umepitisha mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha unaowaingizia wahusika faida ya dolla billioni 80 kwa mwaka, kwa kura 154 zilizounga mkono na kura 3 kutoka Syria, Korea ya Kaskazini na Iran zilipinga muswada huu!
All the contents on this site are copyrighted ©.