2014-06-11 07:55:20

Komesheni nyanyaso za kijinsia!


Kadiri ya takwimu zilizotolewa na "Chama cha Save the children" zinaonesha kwamba, asilimia 80% ya watu wanaonyanyasika kijinsia ni watoto, ambao ni sawa na watoto takribani millioni 30. Chama cha Save the Children kinawataka wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa kimataifa unaolenga kudhibiti na hatimaye kufuta kabisa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa vita na machafuko ya kijamii kuhakikisha kwamba, wanalivalia njuga tatizo hili ambalo ni ukiukwaji wa haki msingi za binadamu.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha machafuko ya kisiasa na hatimaye vita Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, kumekuwepo na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa asilimia 40%, kiasi kwamba, leo hata watoto wadogo wanatambua madhara ya vitendo vya kubakwa na unyanyasaji wa kijinsia walivyofanyiwa na askari.

Hali hii pia imejitokeza kwa namna ya pekee nchini Syria, ambako zaidi ya watu 38, 000 wanahitaji msaada wa kimataifa kutokana na athari za unyanyasaji wa kijinsia walizokumbana nazo. Vitendo kama hivi nchini Liberia viliwahusisha watoto waliokuwa na umri chini ya miaka 17. Watoto wanabakwa na kunyanyaswa kijinsia katika kambi za kijeshi, maeneo ambayo kimsingi yalistahili kutoa ulinzi na usalama kwa wato hawa.

Mambo bado ni mabaya sana nchini DRC watoto na wanawake wanabakwa kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Save the Cildren inasema mkutano wa kimataifa uliofunguliwa hapo tarehe 10 hadi tarehe 13 Juni, 2014 unaodhamiria kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia unapaswa kuibua mikakati itakayosaidia kuwalinda watoto na wanawake wanaodhalilishwa kijinsia wakati wa vita.

Nyanyaso za kijinsia ni dhana pana inayojumuisha pamoja na mambo mengine ubakaji, biashara ya ngono, biashara haramu ya binadamu. Vitendo vyote hivi vinakwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.