Ndugu yako uko wapi? Ndiyo kauli mbiu inayoongoza barua ya kichungaji ya Baraza la
Maaskofu Eritrea iliyochapishwa hivi karibuni, inayogusia kwa namna ya pekee: maadhimisho
ya Mwaka wa Imani na umuhimu wake katika maisha ya waamini; hali hali wanayokabiliana
nayo wananchi wa Eritrea katika kipindi hiki; maafa yanayoendelea kutokea kwa wahamiaji
wanaozama maji baharini wakitafuta maisha bora zaidi; ubora wa maisha nchini Eritrea.
Maaskofu wanachambua
hali ya kisaikolojia na kimaadili miongoni mwa wananchi. Katika maisha ya kijamii
wanazungumzia kuhusu familia na umuhimu wa kuboresha maadili, utawala wa sheria, elimu
na uchumi. Maaskofu wanapembua hali ya maisha ya kiroho na kimaadili miongoni mwa
wananchi wa Eritrea kwa kugusia mzizi wa dhambi na hatimaye umuhimu wa kuanza mchakato
wa ujenzi wa misingi ya amani na utulivu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea
likisukumzwa na imani limeamua kuwaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema
barua ya kichungaji inayowachangamotisha kusimama kidete kujenga umoja, urafiki na
mshikamano wa karibu zaidi na Yesu Kristo kwa kuongozwa na changamoto zilizotolewa
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kichungaji, Mlango wa
Imani, “Porta Fidei”, ili waamini wote waweze kuimarika katika imani kwa Kristo na
Kanisa lake pamoja na kuendelea kuwatangazia watu Injili ya Furaha kama anavyokazia
Baba Mtakatifu Francisko, kwani kuna furaha kubwa katika imani.
Maaskofu wanaainisha
maana ya imani, umuhimu wake katika maisha ya waamini pamoja na kuhakikisha kwamba,
imani hii haibaki inaelea katika ombwe bali inamwilishwa katika uhalisia wa maisha
ya watu, ili kuwajengea watu matumaini, kwani Yesu Kristo ndiye njia, ukweli na uzima.
Kwa njia ya imani, watu wanaweza kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa
sura na mfano wa Mungu; wanaweza kuguswa na mahangaiko ya jirani zao ili kuonesha
moyo wa upendo na mshikamano wa dhati, ili kwa pamoja waweze kuonja furaha ya uzima
wa milele.
Wananchi wa Eritrea kimsingi ni watu wenye imani thabiti, wanaotambua
tofauti zao kama utajiri na kwamba, hawa ni watu wenye kiu ya amani ya kudumu, ndiyo
maana Maaskofu wanauliza, Je, ndugu yako yuko wapi? Maaskofu wanatambua kinzani na
migogoro iliyojitokeza nchini mwao na umuhimu wa kutibu madonda haya ya utengano kwa
kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kuwa watu wapya katika maisha ya kiroho, kimaadili
na kihadhara.
Kwa masikitiko makubwa Maaskofu wa Eritrea wanasema kuna biashara
haramu ya binadamu inayoendelea kutesa na kuwanyanyasa watu kwa kuwajengea matumaini
yasiyokuwa kweli na matokeo yake, kuna maelfu ya watu wanaokufa kwa baridi, njaa,
kiu na utupu jangwani na wale wachache wanaobahatika kuvuka jangwa, wanakufa maji
baharini. Eritrea inawalilia watoto wake wote waliokufa wakiwa njiani kutafuta maisha
bora ughaibuni. Bado kuna makundi makubwa ya watu wanaoikimbia Eritrea. Kila mtu anapaswa
kuwwajibika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani yake nchini Eritrea wanasema
Maaskofu.
Je, hakuna uwezekano wa kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa
Eritrea wakiwa nchini mwao? Je, Eritrea inaweza kuwa na amani ya kweli inayohamasisha
Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo? Tatizo la wananchi wa Eritrea kukimbilia
ughaibuni limeendelea kupigwa dana dana na Jumuiya ya Kimataifa, kumbe, umefika wakati
kwa wananchi wa Eritrea kujipanga wenyewe na hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa maendeleo,
kwani huko ambako vijana wanakimbilia, kunawaka moto! Watu wanakufa maji bila utani!
Wananchi
wengi wa Eritrea wanasema Maaskofu wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na
magonjwa, njaa na umaskini mambo yanayowapelekea hata wakati mwingine kukimbilia uhamishoni
wakidhani kwamba, huko pengine wanaweza kupata nafuu ya maisha. Matokeo yake Eritrea
inaendelea kupoteza rasilimali watu na wataalam ambao hawatarudi tena, kwani wengi
wao wanakufa maji baharini, wale wanaobahatika kufika kwenye Nchi ya ahadi, kamwe
hawatarudi tena Eritrea!
Wananchi wengi wa Eritrea hawana uhakika wa usalama
na ubora wa maisha yao kwa siku za usoni, ni watu wanaoteseka kisaikolojia na kimaadili,
kiasi cha kukata tamaa ya maisha. Kuna idadi kubwa ya wazee ambao hawana tena msaada
kutoka katika familia zao kwani wameachwa pweke, hali inayochangia kuzorota kwa uchumi
na huduma; watu wengi wanakabiliana na magonjwa ya kisukari, msongo wa mawazo na magonjwa
ya moyo! Kwa uchungu mkubwa Maaskofu wanasema, hapa kuna mmong’onyoko mkubwa wa maadili
na utu wema.
Maaskofu wanapenda kuwahimiza wanafamilia kutekeleza dhamana na
wajibu wao kikamilifu licha ya matatizo na changamoto zilizopo nchini Eritrea, kwani
familia bora ni msingi wa maendeleo endelevu ya watu, chemchemi ya imani na hekima,
kumbe, kuna haja ya kuimaarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Umefika
wakati kwa viongozi na wananchi wote wa Eritrea kujikita katika toba na wongofu wa
ndani kwa kuchuchumilia: utu na heshima ya binadamu; haki msingi na mafao ya wengi
kwa kuondokana na ubinafsi, rushwa na ufisadi; ubaguzi na upendeleo. Watu wajenge
tabia ya ukweli na uwazi, uwajibikaji pamoja na uchaji wa Mungu, ili kupambana fika
na ukiukwaji wa sheria unaopelekea kutoweka kwa amani na utulivu. Wanasiasa waoneshe
ukomavu katika masuala ya kisiasa kwa kukazia ukweli, uwajibikaji na utawala wa sheria.
Vyombo vya sheria vitekeleze dhamana yake bila upendeleo wala vitisho kwa
kuzingatia Katiba na sheria za nchi. Wanasiasa wakuze na kuimarisha utamaduni wa kujadiliana,
kusikilizana na kutafuta ukweli kwa pamoja hata katika tofauti zao. Vijana wajengewe
uwezo wa kupambana na maisha yao kwa njia ya elimu makini inayojikita katika maendeleo
ya sayansi na teknolojia na kwamba, Kanisa litaendelea kushirikisha utajiri, uzoefu
na mang’amuzi yake katika sekta ya elimu nchini Eritrea.
Uchumi wa nchi hauwezi
kuendelea kutegemea msaada unaotumwa na wananchi wa Eritrea wanaoishi ughaibuni, bali
kuna haja ya kufufua mikakati na sera makini za uchumi kwa kuboresha tija na uzalishaji
katika sekta ya kilimo, viwanda na huduma pamoja na kuhakikisha kwamba, walau kuna
fursa za ajira ili kuongeza pato ya wananchi kuweza kuwa na nguvu ya manunuzi.
Maaskofu
wanawaalika waamini na wananchi wa Eritrea katika ujumla wao kufanya toba na wongofu
wa ndani, ili kuboresha maisha yao ya kiroho na kimaadili; kwa kukuza dhamiri nyofu
na uchaji wa Mungu. Kwa njia hii, watu wanaweza kumwogopa Mwenyezi Mungu na kuwajali
jirani zao! Vinginevyo, biashara ya binadamu na viungo vyake itaendelea kushamiri;
ngono na utumwa mamboleo yatakuwa ni mambo ya kawaida; uchu wa mali na madaraka yatakuwa
ni mapambo ya wengi na matokeo yake ni kuanguka kwa taifa!
Baraza la Maaskofu
Katoliki Eritrea linahitimisha barua yake ya kichungaji kwa kuwataka watu wajifunze
kuikimbia dhambi na nafasi zake; wajikite katika hija ya haki, amani na upatanisho
wa kitaifa ili kuponya madonda ya utengano, uchoyo na ubinafsi.
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.