2014-06-11 06:41:58

Chezeni kwa ajili ya maisha!


Mashindano ya Kombe la Dunia kwa Mwaka 2014 yataanza kutimua vumbi huko Brazil kuanzia tarehe 12 Juni hadi tarehe 13 Julai, wakati mshindi wa Kombe la Dunia atakapoibuka kidedea na kukata mzizi wa fitina katika utandazaji wa kabumbu duniani. RealAudioMP3

Hili ni tukio ambalo lina mvuto mkubwa kwa mamillioni ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kila mtu akiwa na lengo lake maalum. Waswahili wanasema, kwenye msafara wa Mamba hapo, Kenge hakosekani!

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linasema, linaendelea kufuatilia maandalizi na hatimaye Mashindano ya Kombe la Dunia kwa umakini mkubwa, kwani hili ni tukio la kimataifa, litakalowakutanisha watu wa kila aina. Hiki ni kipindi cha kuonesha upendo na mshikamano wa kidugu, kwani michezo ni udugu na upendo. Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linapenda kutoa salam za rambi rambi kwa wale wote ambao wamewapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao wakati wa ujenzi wa Uwanja wa Mashindano ya Kombe la Dunia.

Maaskofu wameandika ujumbe unaoongozwa na kauli mbiu “Chezeni kwa ajili ya Maisha” na wanawalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika kampeni ya Mashindano ya Kombe la Dunia kwa kusimama kidete kupinga biashara harem ya binadamu, inayoambatana na matukio makubwa kama haya ya Mashindano ya Kombe la Dunia. Wananchi watambue na kuheshimu thamani ya michezo, kwa ajili ya kupata afya bora pamoja na kuwaheshimu na kuwathamini watu wengine ndani ya Jamii.

Mchezo wa Kabumbu ni sehemu ya vinasaba vya wananchi wa Brazil, wakiwa uwanjani, utachoka na roho yako wanasema Maaskofu! Hii ndiyo furaha ambayo wananchi wa Brazil wanataka kuwashirikisha walimwengu wakati wa Mashindano ya Kombe la Dunia.

Maaskofu Katoliki kutoka Brazil wakitambua dhamana yao katika mchakato wa Uinjilishaji, wanaendelea kuhimiza umuhimu wa michezo kama chemichemi ya furaha, upendo na mshikamano wa dhati. Wananchi wa Brazil waoneshe ukarimu, furaha na upendo kwa watu wote watakaofika nchini mwao kushuhudia wanamichezo wakitandaza kabumbu ya nguvu, bila kuwasahau mashabiki na watazamaji wa kawaida. Wageni wote hawa waonje utajiri wa Brazil katika utofauti wake, kwa kuthamini: haki, amani na utulivu, hata kama mchezo wa Mpira wa miguu unafumbata pia mambo ya kiuchumi na fahari zake.

Baraza la Maaskofu Katoliki linaonesha masikitiko yake kutokana na maandamano yaliyojitokeza nchini humo hivi karibuni kwa wahusika kutoheshimu wala kuzingatia haki msingi za wanyonge ndani ya Jamii. Umaskini bado umeendelea kuwaandama wananchi wengi wa Brazil, licha ya rasilimali na utajiri mkubwa waliobahatika kuwa nao na badala yake, kinzani za kijamii zimeendelea kutawala badala ya kuhakikisha amani na utulivu, utu na heshima ya binadamu.

Inasikitisha kuona kwamba, kutokana na Mashindano ya Kombeo la Dunia, kuna familia nyingi zimelazimika kuhama katika makazi yao ili kupisha ujenzi wa wa miundo mbinu kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Dunia jambo ambalo linaonesha uvunjifu wa haki msingi za binadamu.

Mashindano haya yasiwe ni kisingizio cha ukosefu wa haki na usawa pamoja na uharibifu wa mazingira. Mafanikio ya Mashindano ya Kombe la Dunia nchini Brazil yatapimwa si tu kutokana na faida kubwa itakayopatikana, bali katika utekelezaji wa haki, amani, ulinzi na usalam; kwa kuheshimu haki ya uhuru wa mtu kujieleza.

Serikali inapaswa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kudhibiti biashara haram ya binadamu na utumwa mamboleo; vitendo vya ubaguzi wa rangi pamoja na mabo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil linavyokamilisha ujumbe wake kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Dunia nchini Brazil kwa Mwaka 2014.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.