Utume wa Kanisa miongoni mwa Zingari unahitaji sera na mikakati mipya ya shughuli
za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa jamii hii, ili kubomo kuta za utengano:
kijamii, kisiasa na kitamaduni ndani ya Jamii.
Hivi ndivyo
anavyofafanua Kardinali Antonio Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la wahamiaji
na watu wasiokuwa na makazi maalum wakati wa kufunga kongamano la kimataifa lililowashirikisha
wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kwa pamoja kupembua mikakati ya Kanisa
na Zingari ili kutangaza Injili pembezoni mwa Jamii.
Lengo la kongamano hili
lilikuwa ni kuchambua tena mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama
Kanisa kwa ajili ya Zingari, ili iweze kuwa na mguso na mashiko kwa wahusika kama
sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya katika mazingira yao. Wajumbe wamepembua historia
ya Zingari tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Papa
Paulo VI alipokutana na Zingari huko Pomezia kunako tarehe 26 Septemba 1965, huu ukawa
ni mwanzo wa shughuli za kichungaji kwa Zingari.
Kwa namna ya pekee, wajumbe
wameangalia changamoto za kichungaji zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika
Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium. Wajumbe wamegusia
matatizo, changamoto na fursa ambazo zinawafanya Zingari wakati mwingine kutengwa
na jamii wanamoishi hasa katika masuala ya afya na tiba; makazi, fursa za ajira na
elimu.
Kuna mikakati inayoendelea kufanyiwa kazi ili kuwawezesha watoto wa
Zingari kwenda shule, umuhimu wa kuzingatia utawala wa sheria na amani kati ya jamii
husika. Makanisa mahalia yanaendelea kuhimizwa kuweka mikakati ya kichungaji kifamilia
na kirika ili kuwawezesha Zingari kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Utamadunisho wa imani katika mazingira wanamoishi Zingari ni kati ya changamoto
zilizoainishwa na wajumbe wakati wa mkutano wao uliohitimishwa mjini Vatican. Ni matumaini
ya wajumbe hawa kwamba, Watumishi wa Mungu Emilia Fernàndes na Juan Ramòn Gil, Mashahidi
wa Kizingari wataweza kutangazwa kuwa Wenyeheri na Mama Kanisa.
Kumbu kumbu
ya miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipowatembelea Zingari Pomezia ni tukio muhimu sana
katika mikakati ya kichungaji inayotekelezwa na Kanisa tangu wakati huo, kwani Zingari
wanaweza kukutana na ndugu na jamaa wanaopenda kama alivyopenda Yesu mwenyewe! Hivi
ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alivyokazia wakati alipokutana na Wajumbe wa kongamano
la kimataifa kuhusu utume wa Kanisa miongoni mwa Zingari sehemu mbali mbali za dunia.
Imetayarishwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.