Kanisa Katoliki linaendelea kuwekeza katika malezi na makuzi ya watoto kwa kuwajengea
maisha ya sala, umoja, udugu na mshikamano kwa kutambua kwamba, watoto ni taifa la
kesho, kumbe, changamoto kubwa iliyoko mbele ya Familia ya Mungu ni kuhakikisha kwamba,
kwa pamoja inashiriki katika kuwalea watoto ili wakue katika imani ya Kikristo, maadili
na utu wema!
Mashirika
ya Kipapa ya Kimissionari nchini Tanzania kuanzia tarehe 12 – 16 Juni 2014 yatafanya
Kongamano la Kitaifa la Utoto Mtakatifu, Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi na kuongozwa
na kauli mbiu “Nimtume nani? Niko hapa nitume mimi”. Rai ya Mashirika ya Kipapa ya
Kimissionari nchini Tanzania inasema kwamba, watoto waliolelewa katika imani ya Kikatoliki
ni nguzo za Kanisa Katoliki na Jamii nzima.
Katika kongamano hili la kitaifa
litakalowajumuisha watoto kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania litajadili pamoja
na mambo mengine kuhusu: Mtoto na imani; Watoto na athari za utandawazi; Watoto na
maisha ya Sakramenti hasa Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Haki za watoto na wajibu
wao kwa wazazi na walezi; wajibu wa wazazi katika malezi ya watoto; Watoto na maisha
ya watakatifu; Watoto na utume wa umissionari; Watoto na miito mitakatifu.
Watoto
pia wataangalia wajibu wao kama sehemu ya matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa imani
uliotishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kuadhimishwa kwa kishindo na
Papa Francisko. Askofu Castor Msemwa wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi ndiye mwenyeji
wa kongamano la kitaifa la Utoto Mtakatifu nchini Tanzania.