Mashindano ya Kombe Dunia kwa Mwaka 2014 yanaanza kutimua vumbi kwenye viwanja kumi
na viwili kutoka Rio hadi Manaus nchini Brazil. Hiki kitakuwa ni kipindi cha kusuka
na kunyoa. Mtawasikia mashabiki wa mpira wa miguu wakishangilia na kulilia timu zao
za kitaifa! Ni mambo ya kawaida!
Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwa kushirikiana
na wadau mbali mbali wametoa kanuni kumi zinazolenga kuisaidia Brazil ili kujenga
usawa na haki kwa wote. Jambo la msingi kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba, inatoa
fursa za ajira bora kwa wote; watu wapewe nafasi ya kuhitimu masomo, uhakiki wa demokrasia
kwa njia ya haki; wananchi wa Brazil wanasubiri kuona mabadiliko katika sekta ya kilimo
na uzalishaji; ulinzi na usalama kwa vijana na watoto; udumishaji wa utamaduni wa
tofauti miongoni mwao.
Serikali haina budi kujifunga kibwebwe kuhakikisha
kwamba inapambana kufa na kupona na vitendo vya rushwa, wizi naufisadi kwa kujikita
katika ukweli na uwazi; Serikali haina budi kujielekeza zaidi katika maboresho ya
masuala ya kijamii kwa kukazia afya kwa wote.
Kwa njia hii, Serikali ya Brazil
itakuwa inajibu changamoto kubwa ambazo zimekuwa zikijitokeza nchini humo kutokana
na gharama kubwa za kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia kwa Mwaka 2014 yanayoanza
kutimua vumbi nchini Brazil kuanzia tarehe 12 Juni 2014.