Bwana Abdel-Fattah el-Sissi, mwenye umri wa miaka 59, Jumapili tarehe 8 Juni 2014
ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Misri baada ya kuibuka kidedea katika kinyang'anyiro
cha uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Misri hivi karibuni. Katika hotuba yake amekazia
umuhimu wa wananchi wa Misri kushiriki kikamilifu katika mchakato wa upatanisho wa
kitaifa, ili kuponya madonda ya chuki na utengano kwa kukazia utawala wa sheria.
Anasema,
atalivalia njuga tatizo la rushwa na ufisadi nchini Misri, ataendelea kukazia uhuru,
haki jamii na utengenezaji wa fursa za ajira, ili watu waweze kujipatia riziki yao
pamoja na kukuza utamaduni wa kusikilizana kama sehemu ya mafao ya wengi, ustawi na
maendeleo ya Misri.
Katika utawala wake, Misri inapenda kujielekeza zaidi
katika ukuzaji wa haki na utulivu katika Ukanda wa Nchi za Kiarabu kwa kuwataka wananchi
wa Misri kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kukuza na kudumisha haki, uhuru na
umoja wa kitaifa.
Rais El-Sissi anakuwa ni Rais wa nane kuingia madarakani
tangu kulipotokea mapinduzi ya kijeshi kunako mwaka 1953. Kwa miaka mingi Misri imeongozwa
na Marais wanaotoka jeshini, isipokuwa Rais Morsi aliyeng'olewa madarakani na Marais
wengine ambao walikuwa ni raia walioongoza katika kipindi cha mpito!