2014-06-08 09:38:14

Wasaidieni wafungwa kujirekebisha!


Haki ya kweli inajikita katika mchakato unaolenga kusahihisha, kuboresha na kuelimisha makosa yaliyojitokeza badala ya kulaani na kuhukumu! Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anatahadharisha wajumbe wa wanaoshiriki kongamano la kumi na sita kimataifa la wanasheria kutoka Amerika ya Kusini sanjari na kongamano la tatu la sheria kimataifa.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sheria inaheshimu na kuzingatia utu wa mwanadamu na haki zake msingi pasi na ubaguzi pamoja na kuhakikisha kuwa, wanyonge ndani ya jamii wanalindwa zaidi.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, magereza Amerika ya Kusini yamefurika kwa wafungwa, hali ambayo inawanyanyasa na kuwadhalilisha wafungwa ambao wanahukumiwa adhabu mbili kwa mpigo! Kuna haja ya jamii kutambua kwamba, wakati mwingine kinzani na mapambano ya kijamii ni matokeo ya ukosefu wa haki na usawa katika masuala ya kiuchumi na kijamii, hali ambayo inawafanya baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi mwao.

Adhabu kali bado hazijafanikiwa kupunguza vitendo vya uhalifu na makosa ya jinai katika jamii nyingi. Hapa kuna haja ya kupambanua kati ya haki na mchezo wa kulipizana kisasi, kwa kuangalia uwezekano wa mfungwa kujirekebisha na kuanza upya hija ya maisha yake ndani ya jamii.All the contents on this site are copyrighted ©.